Na Veronica Mwafisi,TimesMajira Online,Muheza
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Deogratius Ndejembi amewaelekeza Viongozi wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa Shule ya Sekondari Kwemkabala unaogharimu shilingi milioni 66 zilizotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) baada ya kutoridhika na maendeleo ya ujenzi huo.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua ujenzi wa shule hiyo akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF katika Wilaya ya Muheza.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa Shule hiyo,Ndejembi amesema, kiasi cha fedha kilichotumika mpaka sasa hakiendani na kazi iliyofanyika na hii inatokana na ushauri au usimamizi mbaya uliotolewa juu ya ujenzi wa shule hiyo.
“Mhandisi anayesimamia ujenzi wa shule hii hakushauri vizuri kuanzia kwenye msingi mpaka ulipofikia, akiwa kama mtaalam, alitakiwa aangalie anachokishauri, kinachojengwa na thamani ya fedha iliyotolewa, hivyo Mkurugenzi na Watendaji wa TASAF muangalie namna gani ya kufanya ili jengo hili liweze kukamilika kwa ubora,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Ndejembi ameongeza kuwa, kiasi cha fedha kilichobaki ambacho ni shilingi milioni 39 hakiwezi kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwa ubora kwani sehemu iliyobakia ni kubwa na fedha zilizobaki ni kidogo.
Ndejembi amesema Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo, hivyo hafurahishwi kuona zikitumika vibaya.
Ujenzi wa shule hiyo unajumuisha vyumba viwili vya madarasa, ofisi na matundu matano ya vyoo.
More Stories
Maghorofa Kariakoo mikononi mwa Tume
ITA chatakiwa kutoa mafunzo ya viwango vya juu na kasi ya maendeleo ya Kisayansi
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi