November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nape:Serikali imeweka vifaa vya kisasa kurahisisha huduma za afya

Mwandishi wetu,Timesmajira online

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Nape Nnauye amesema serikali imewekeza katika miundombinu ya vituo vya afya kwa kuhakikisha inakuwa na vifaa vya kisasa ili kurahisisha huduma ya afya kwa wananchi hususani wenye kipato cha chini.

Nape ameyabainisha hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na uongozi wa kampuni ya bima ya Jubilee, Airtel na Axieva kuhusu huduma mpya ya bima ya gharama nafuu inayotarajiwa kuhudumia watu zaidi ya milioni 17.5.

Amesema serikali ipo tayari kumuunga mkono mtu yeyote atakayetumia teknolojia kuokoa maisha ya watu wanyonge.

“Ili kuhakikisha kila Mtanzania wa kipato cha chini ananufaika na maendeleo yanayotendwa na serikali, kila mmoja aone namna ya kutumia teknolojia,natamani kuona jinsi Tehama ikitumika kuokoa maisha ya watu na itakavyobadilisha maisha yao hususani katika huduma za afya,”amesema Nape.

Amesema watu wengi wakiwekeza kwenye afya kupitia teknolojia watasaidia kutoa mchango kwa Wizara ya Afya na kuokoa fedha nyingi za matibabu ndio maana hata serikali imelenga kwa kila Mtanzania kupata bima ya afya kwa gharama nafuu.

Aidha aliiupongeza uongozi wa kampuni ya Airtel Tanzania, Bima ya Jubilee na kampuni ya Tehama. ya Axieva kwa kuanzisha bidhaa mpya ya Afya Bima ambayo ni nafuu kwa wateja wa Airtel Tanzania.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Jubilee, Dk. Harold Andamson amesema bima hiyo itakuwa ya gharama nafuu na kila mtanzania ataweza kuitumia mara tu atakapolipa kupitia Airtel Money.

Amesema bima hiyo itatumika kwa zaidi ya vituo 642 ambavyo ni vya serikali lengo likiwa kuwafikia watu wenye kipato cha chini kuweza kunufaika na bima hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Airtel Money, Andrew Rugamba amesema ushirikiano wa kampuni hizo tatu ni mkakati uliolenga kuleta mapinduzi katika mazingira ya bima ya afya kwa kutoa huduma nafuu zinazoendana na soko ambazo upatikanaji wake ni rahisi kwa Watanzania wote.