April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwili wa Marehemu wafukuliwa kwa uchunguzi

Na Esther Macha, TimesMajira Online ,Mbarali

MWILI wa Marehemu Tulizo  Konga (38) aliyefariki machi  25,mwaka huu  na kuzikwa machi 28,mwaka huu  umefukuliwa kwenye makaburi ya Igumbilo yaliyoko Kata ya Chimala, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Mwili huo umefukuliwa  mara baada ya ndugu wa Marehemu kudai kulikuwa na utata wa kifo chake.

Zoezi la kufukua kaburi ambalo lilisimamiwa na Jeshi la Polisi  pamoja na madaktari lilifanyika jana baada ya Mahakama kutoa kibali cha kuruhusu mwili wa marehemu ufukuliwe na kisha ufanyiwe uchunguzi kwa madai ya utata wa kifo.

 Utata huo umetokea baada ya ndugu wa Marehemu kudai kuwa hawakupata taarifa za kuumwa za  Marehemu Tulizo kutoka kwa mume wake, Kelvin Mwanjemba.

Familia ya Marehemu imesema kuwa  sababu ya kutaka kufukuliwa kwa kaburi la ndugu yao ni baada ya mume kutotoa taarifa ya kuumwa na kifo  badala yake kuzipata kwa majirani.

Msemaji wa familia, Msafiri Mlowezi amesema licha ya kuzisikia taarifa za kifo kutoka kwa majirani lakini pia walizuiwa kuuona na kuuaga mwili wa marehemu kabla ya kuzikwa hali iliyosababisha kuwa na maswali mengi.

“Kutokana na vitendo hivyo familia ya Tulizo walikubaliana kuongea na vyombo vya sheria wakitaka mwili wa marehemu ufukuliwe ili kufahamu kama kweli marehemu alifariki dunia kwa ugonjwa au aliuawa,”amesema na kuongeza

“Baada ya  kupata kibali cha kufukua mwili wakazi wa Igumbilo, ndugu wa marehemu   walifukua kaburi  na wakiwa eneo la makaburi waliomba kufunua jeneza ili kuangalia mwili wa ndugu yao kabla ya kupelekwa mochuari kwa ajili ya uchunguzi kama walivyotaka kubaini chanzo cha kifo chake,”amesema Mlowezi

Mwili wa marehemu ulipelekwa Hospitali ya Chimala kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi majira ya saa moja usiku Juni 30,mwaka huu ikiwa chini ya    jopo la Madaktari wa serikali na familia kwa kushirikiana Jeshi la Polisi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amewaomba ndugu wa marehemu Tulizo kuendelea kusubiri taarifa ya uchunguzi kutoka kwa wataalam  na kuhakikishia kuwa haki itaendeka endapo kutokuwa na chochote kitu chochote.

Matei amesema Jeshi la Polisi haliwezi kumkamata mume wa Marehemu, Kelvin Mwajemba kama ndugu wa marehemu wanavyotaka kwa madai kuwa hakuna uthibitisho wowote unaonesha kuwa alihusika na tukio hilo na kudai ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu ndio itatoa majibu.