November 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwigulu kufunga maadhimisho ya wenye ulemavu Mwanza

Na Penina Malundo,TimesMajira

WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, Desemba 3, mwaka huu, mkoani Mwanza.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, Serikali inatarajia kuzindua nyaraka nne muhimu zinazolenga kuimarisha haki, ustawi na upatikanaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu, pamoja na kuboresha mifumo ya kuwahudumia katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na Waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema nyaraka zitakazozinduliwa ni Mwongozo wa Kitaifa wa Viwango vya Ufikivu wa Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2026, Mwongozo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Mashauri ya Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2026, Mpango Kazi wa Kuimarisha Usawa katika Upatikanaji wa Huduma za Afya kwa Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2026 hadi 2031 na Ripoti kuhusu Hali Halisi ya Watoto na Vijana Wenye Ulemavu Tanzania ya mwaka 2026.

Amesema mwongozo wa viwango vya ufikivu unalenga kuweka viwango na maelekezo yatakayohakikisha majengo, miundombinu, usafiri, taarifa, mawasiliano na huduma mbalimbali zinakuwa rafiki na kufikika kwa watu wenye ulemavu.

“Hatua hiyo itasaidia kuondoa vikwazo vinavyowazuia kupata huduma na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo, huku ikiimarisha utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura ya 183.

“Kuhusu mwongozo wa usimamizi wa mashauri, tutaweka mfumo wa pamoja wa kutambua, kupokea, kutathmini, kuratibu na kufuatilia mashauri yanayohusu watu wenye ulemavu, ili kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya taasisi zinazohusika na utoaji wa huduma,”amesema

Amesema mpango kazi wa huduma za afya utasaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora, salama na jumuishi kwa watu wenye ulemavu kwa kuondoa vikwazo vya kimawasiliano, kitaasisi na kimtazamo vinavyozuia upatikanaji wa huduma hizo.

Aidha, ripoti kuhusu hali ya watoto na vijana wenye ulemavu itatoa ushahidi kuhusu fursa na changamoto wanazokabiliana nazo katika kupata elimu, huduma za afya, ulinzi na mafunzo ya ujuzi, pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Amesema matokeo ya ripoti hiyo yatasaidia Serikali na wadau kupanga afua zinazozingatia mahitaji halisi ya watoto na vijana wenye ulemavu na kuimarisha ulinzi wa haki zao..

Maadhimisho hayo yanafanyika katika Viwanja vya Magana, jijini Mwanza, kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 3, mwaka huu, yakiandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Serikali ya Mkoa wa Mwanza na wadau mbalimbali wa maendeleo.