November 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jamii yatakiwa kuondoa dhana kukwamisha wanawake kushiriki michezo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, ameitaka jamii kuondoa dhana potofu zinazokwamisha ushiriki wa wanawake katika michezo,.

Hata hivyo alisisitiza umuhimu wa kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha wanawake na wasichana kuonesha vipaji vyao.

Hayo ameyasema wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Riadha ya Wanawake ya Ladies First, msimu wa nane, yaliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Elimu Kibaha
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo.

Amesema, ushiriki mdogo wa wanawake katika michezo unachangiwa na majukumu ya kifamilia, ukosefu wa elimu na fursa za kutosha za michezo kwa watoto wa kike.

Aidha, amesema mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kuibua na kuendeleza vipaji vya wanariadha wanawake kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambao wanaweza kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya kimataifa, yakiwemo ya Jumuiya ya Madola, Afrika na Olimpiki.

Amelitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kwa kushirikiana na wadau wengine, kuimarisha programu za kukuza michezo ya wanawake, kutoa elimu kwa jamii na kuweka mazingira wezeshi.

Pia, amezitaka halmashauri, taasisi za elimu na wadau wa michezo mkoani Pwani kutumia mashindano hayo kuibua vipaji kuanzia ngazi ya shule za msingi.

Magoti ametoa wito kwa kampuni, taasisi na watu binafsi kujitokeza kudhamini michezo ya wanawake, akibainisha kuwa michezo si burudani pekee bali pia ni chanzo cha ajira, uchumi, afya bora na umoja wa kitaifa.

Amewapongeza BMT, JICA, Shirikisho la Riadha Tanzania na mwanzilishi wa mashindano hayo, Kanali Juma Ikangaa, kwa mchango wao katika kuendeleza riadha ya wanawake nchini.