October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa kijiji atuhumiwa kumpa ujauzito mwanafunzi darasa la 6

Na David Magesa, TimesMajira,Magu

MWENYEKITI wa Kijiji cha Ijinga katika Wilaya ya Magu, Badri Juma Masengo (40) anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa darasa la sita wa Shule ya Msingi Ijinga mwenye umri wa miaka 15 jina linahifadhiwa.

Kutokana na kadhia hiyo Jeshi la Polisi Wilaya ya Magu linamshikilia mwenyekiti huyo kwa mahojiano akituhumiwa kutenda kosa hilo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli amesema hakubaliani na hatakubali kuona watoto wa kike wanakatishwa masomo na wanaume wenye uchungu wa ngono wanaohangaika na wanafunzi wakati wanawake wamejazana mitaani na kuonya wenye tabia hiyo na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema, katika wilaya hiyo yapo mambo ya ovyo yanafanywa na baadhi ya walimu, wazazi na jamii kwa kufanya ngono na wanafunzi wa shule na kukatisha ndoto zao za elimu na kuonya hatakubali hayo yaendelee huku akitoa angalizo kwa watumishi wa idara ya polisi na mahakama wanaopindisha sheria sababu ya rushwa kwenye kadhia hiyo hawatabaki salama.

Kalli amesema kuwa, Rais Dkt. John Magufuli amefuta ada kwa shule za msingi hadi kidato cha nne na kurahisha mambo kwa wananchi ambao hawakuwa na uwezo ili kuwawezesha watoto kusoma kwa raha watimize ndoto zao, lakini watu wachache kwa tamaa ya ngono wanawaharibia maisha.

“Ilani ya uchaguzi Ibara ya 80 inaeleza uboreshaji wa elimu kutoka msingi hadi chuo kikuu mtoto asome hadi mwisho hata kama mzazi hana uwezo na serikali inataka wasome kwa raha watimize ndoto zao na hivyo sitawavumilia wanaume wanaojamiana na watoto na nitoe rai kwa idara ya mahakama na polisi watende haki kwa mtoto aliyekatishwa masomo na mwenyekiti huyo ili liwe fundisho kwa wengine wanaokiuka maadili na kuharibu maisha ya watoto,”amesema.

Mkuu huyo wa wilaya amesema tatizo la rushwa kwa baadhi ya watumishi wa mahakama na polisi wasio na uadilifu,linakwamisha juhudi za serikali na kuwataka kuzingatia kauli ya Rais Magufuli wakati akimwapisha Mwanasheria Mkuu.

“Jaji Mkuu wa Tanzania naye alirudia maneno hayo,na mimi leo naelekeza sina shaka na sitaki kuamini kuwa rushwa itatembea kwenye kesi hii,sitaki kuhukumu maana ushahidi uko wazi, hivi mpepelezi katika kesi hii anataka kueleza nini na ninaomba isichukue muda mrefu ili haki itendeke,”amesema Kalli.

Mwanafunzi huyo mwenye ujauzito wa wiki 11 miezi miwili na wiki moja amesema, kwa muda mrefu mtuhumiwa huyo Badri Juma alikuwa akimtongoza ambapo alimfuata nyumbani kwao majira ya saa 6 usiku baada ya wazazi wake kwenda msibani na kumwacha na wadogo zake na kumshawishi kuondoka naye hadi kwake.

Amesema, walipofika nyumbani hapo mtuhumiwa huyo alimvua nguo kisha akampatia sh. 20,000 na kumwingilia,hata hivyo baada ya kutimiza haja zake alimnyang’anya fedha hizo na kumrejesha tena kwao usiku huo huku akimpa ahadi ya kumpa matumizi na nguo, lakini hakutimiza ahadi hiyo.

Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Magu, Glory Vicent Mtui amempongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa jinsi anavyoshughulikia changamoto ya mimba kuhakikisha wahusika wanakamtwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuahidi hawatafumbia macho suala la mwanafunzi huyo licha ya baadhi ya wazazi kuwaficha wahalifu kwa kupewa rushwa sababu ya mazingira magumu na umasikini.

“Tangu Januari, mwaka huu takwimu za mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi ni 28 na siamini mzazi yeyote anafurahia mwanaye kukatishwa masomo na hili tatizo la mimba tutafanya kazi ya kukabiliana nalo na kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa mahakamani na hadi sasa zipo kesi 28 baadhi ziko mahakamani na zingine watuhumiwa wamekimbia ama kuachiwa sababu ya changamoto ya rushwa kwa mashahidi,”amesema Mtui.

Aidha, Afisa Mtendaji wa Kata Kahangara, John Clavery Mabati amesema kuwa, mtuhumiwa alipokamatwa na kuhojiwa alikiri kufanya ngono na kumpa ujauzito mwanafunzi huyo na ili kujinasua na mkono wa sheria alijaribu kumshawishi kwa kumpa rushwa ya sh.milioni mbili akaikataa.

Amedai, kabla watu waliotumwa kumkamata mtuhumiwa huyo walihongwa kabla ya kumkamata Novemba 4, mwaka huu ambapo alimfahamisha DC (Mkuu wa Wilaya) naye akaagiza asiachiwe ndipo wakamfikisha polisi kwa hatua za kisheria.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ijinga, Ncheyeki Casmir amesema, mwanafunzi huyo ambaye alikuwa miongoni mwa 10 waliopelekwa kwenye vipimo vya mimba,alibainika kuwa na ujauzito na hakuwahi kuwaeleza wazazi kitendo alichofanyiwa.

Amesema, walipomhoji mwanafunzi huyo aliwaeleza kila kitu kuhusu suala hilo na kwamba siku wazazi wake wakiwa wamekwenda kulala msibani usiku mtuhumiwa alifika nyumbani kwao akamshawishi na kumchukua usiku huo na kwenda naye nyumbani kwake na kumwingilia huku akimpa ahadi ya kumhudumia.

Naye mama mzazi (jina linahifadhiwa) wa mwanafunzi huyo amesema, licha ya kuwa wanalala nyumba moja na binti yake hakuwahi kumweleza lolote kuhusu Badri na alipata taarifa ya ujauzito kutoka kwa walimu baada ya kuitwa shuleni na kuelelezuwa binti yake ana ujauzito wa wiki 11.