April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenezi Shaka aungana na waislamu katika swala ya Eid Al-Fitri-Kigoma

Na Mwandishi wetu ,Timesmajira,Online

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka ameshiriki swala ya Eid Al-Fitr na waumini wa Dini ya Kiislam Mkoa wa Kigoma iliyosaliwa katika Uwanja wa Stendi Mpya ya Ujiji-Kigoma mapema leo tarehe 14 Mei 2021.

Swala hiyo iliyoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Kigoma Sheikh Hassan Kiburwa ilihudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Juma Duni Hajji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Suleiman Jafo, Mbunge wa Jimbo la Kigoma mjini, Kilumbe Shaban Ng’enda, Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hillary na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma Maryam Ditopile.

Katika salamu zake za Eid Al-Fitr kwa waumini wakati wa Swala, Mwenezi Shaka amefikisha salamu za Eid kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambapo amewaambia waumini kuwa anawapenda na anawatakia heri na furaha katika siku muhimu Duniani ya kusherekea sikukuu.

Mwenezi Shaka amewaomba waumini kuliombea Taifa pamoja na kumuomba Mwenyezi Mungu amjaalie Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, ampe Afya njema, maono na msimamo thabiti katika kuiongoza nchi yetu.

Aidha, Mwenezi amewataka wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kuzalisha ili kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa Taifa, sambamba na kutimiza kutunza na kuimarisha hali ya amani, utulivu, umoja na Mshikamano katika nchi yetu.