April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanza kumaliza changamoto ya KKK kwa wanafunzi wa darasa la kwanza, la pili mwezi Septemba mwaka huu

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Imeelezwa kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu Mkoa wa Mwanza,utakuwa umeondoa changamoto ya wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili ambao hawamudu kusoma,kuandika na kuhesabu (KKK).

Ambapo mpaka sasa Mkoa una wanafunzi 21,000 wa darasa la kwanza na la pili na la tatu katika shule za msingi ambao hawamudu KKK.Kwani KKK ni tatizo kubwa sana,kama mwanafunzi hakivuka darasa la pili akaingia la tatu hajui kusoma,kuandika na kuhesabu maana yake hayo masomo mengine yote hatoyaelewa.

Akizungumza na TimesMajira Online ofisini kwake Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martin Nkwabi, ameeleza kuwa,Desemba mwaka 2021,walikuwa na wanafunzi 37,000 waliokuwa hawamudu KKK,katika madarasa hayo lakini kwa kipindi cha mwaka mmoja wamepunguza idadi hiyo mpaka kufikia 21,000.

Nkwabi ameeleza kuwa,walifanya jitihada za kupunguza idadi hiyo,ambapo walikuwa na orodha ya wanafunzi hao ambao hawamudu KKK tatu walitafuta orodha yao kisha Mkoa walikutana na kuwakabidhi Maofisa Elimu Kata orodha ambayo inataja jina la mwanafunzi,darasa na shule anayotoka.

Ambapo waliwaagiza Maofisa Elimu Kata kuweke mkakati maalumu kwa ajili ya kuhakikisha wanafunzi hao wanaweza kumudu kusoma,kuandika na kuhesabu,hatua hiyo ndio imewasaidia ambao wengine walioanzisha madarasa rekebishi,wengine waliamua kubadilisha walimu na kuweka walimu wengine huku wengine wanawafundisha kwa muda tofauti lengo ikiwa ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapungua.

Ameeleza kuwa kila baada ya miezi miwili,wanatuma mtu anazifikia shule na kupima,ili kufahamu maendeleo ya watoto waliokuwa hawamudu KKK kama idadi yao imepungua kwa kuwaita majina yao na kuwapima kwa kusoma,kuhesabu na kuandika.

Hivyo ameeleza kuwa wanataka mwanafunzi asivuke darasa la pili bila kujua kusoma,kuandika na kuhesabu ambapo wameamua kuimarisha ufundishaji wao kwanza kuhakikisha Mwalimu anayefundisha KKK kwa darasa la kwanza ni yule mwenye uwezo wa kufanya hivyo.

Ameeleza kuwa Walimu wanaofundisha darasa la kwanza na la pili ni wenye uwezo na wakifanya ufuatiliaji wakakuta Mwalimu Mkuu ameweka Mwalimu goigoi mwenye sifa mbaya darasa la kwanza na la pili,atakuwa amepoteza sifa za kuwa Mwalimu Mkuu.

Hata hivyo amefafanua kuwa ufundishaji wa KKK unapita katika hatua kuu tatu,kwanza mwanafunzi anafundishwa kuandika hewani,akimudu kuandika hewani Mwalimu anamwambia twende ukaandike kwenye udongo hiyo ni hatua ya pili na akimudu anakwenda kwenye hatua ya tatu ya kuandika kwenye daftari lenye mistari mikubwa na midogo kisha akimudu katika daftari hilo ana hamia kwenye daftari lenye mistari ya kawaida.

“Tumegundua baadhi ya walimu wengine hawana uwezo wa kufundisha vizuri KKK kwaio tumewatafutia walimu wa kuwafundisha yani walimu wa kuwafundisha walimu wa madarasa ya chini ya la kwanza na la pili namna ya kuwafundisha wanafunzi hao chini ya programu ya Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini(MEWAKA),”ameeleza Nkwabi.

Hivyo ameeleza kuwa wanataka kila Kata iwe na kituo cha mafunzo hayo ili kuwajengea walimu uwezo ambao hawana uwezo mzuri wa kufundisha masomo yao na hii imewasaidia sana mfano Halmashauri ya Buchosa na Sengerema wamefanya vizuri sana katika programu ya MEWAKA, ambapo Mwalimu mwenye uwezo anamsaidia asiye na uwezo kuwa akitaka kufundisha fundisha namna hii ni mafunzo mazuri ambayo yameratibiwa na ofisi ya elimu.

“Tunaamini kufikia Septemba mwaka huu kwa kutumia utaratibu wetu huu wa kumkabidhi Ofisa Elimu Kata majina na utaratibu wetu wa madarasa ya awali,la kwanza na la pili yanafundishwa na walimu mahili wanaopenda kufundisha na kuipenda kazi yake,kuwai kazini na mwenye kufanya kazi yake bila kusimamiwa tutakuwa tumemaliza tatizo hili kwa Mkoa wa Mwanza,”ameeleza Nkwabi.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana ‘B’ ,Theresia Silas akizungumza na TimesMajira Online ilipotembelea shuleni hapo, ameeleza kuwa katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Halmashauri ya Jiji la Mwanza limeweka utaratibu wa kuwapa mafunzo walimu wote wale wanahusika na KKK.

“Kama shule tupo kwenye utaratibu wa kuhakikisha kwamba wale wote ambao hawafahamu zile KKK wanazifahamu kwa ustadi unaohitajika kupitia juhudi za walimu na matumizi sahihi ya zana za kufundishia,”ameeleza Mwalimu Theresia.

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana’A’ Anadoreen Rugaimukamu, ameeleza kuwa mpango wa kuhakikisha wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanazifahamu KKK,kwanza ni wanao walimu wanaofanya kazi hiyo kwa madarasa hayo.

“Walimu wa elimu ya awali anapofundisha watoto,baada ya muda anakaa na wale ambao wanahitaji kuendelea kupata muda wa ziada kwa ajili ya KKK,na darasa la kwanza na la pili vilevile,yapo madarasa rekebishi ya awali.Aidha yanatangulia darasa au baada ya darasa la kawaida,kwa ajili ya kusaidia wasiojua hizo KKK tunaimani kufikia Novemba tutakuwa na watoto wote wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu,”ameeleza Rugaimukamu.

Naye mmoja wa wananchi jijini Mwanza, Agnes Lucas, ameeleza kuwa katika kumaliza changamoto hiyo ya Kwa wanafunzi kutomudu KKK, wazazi washirikiane na walimu kwa kuhakikisha watoto wao wanaporejea nyumbani wanatenga dakika chache za kumfundisha kusoma,kuandika na kuhesabu.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza Martin Nkwabi,akizungumza na TimesMajira Online ofisini kwake, jijini Mwanza.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana’B’,Theresia Silas, akizungumza na TimesMajira Online shuleni hapo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Nyamagana’A’, Anadoreen Rugaimukamu akizungumza na TimesMajira Online shuleni hapo.