October 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanga Hakika Benki yatoa upimaji macho bure

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

BENKI ya Mwanga Hakika Tawi la Mwanza, kwa kushirikiana na Hospitali ya Dr.Agarwals, imetoa huduma ya upimaji wa macho bure kwa wananchi wa Jiji la Mwanza ikiwa ni sehemu ya shughuli za Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Akizungumza Oktoba 8, 2026 katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Mwanza, Meneja wa Kanda wa Mwanga Hakika Benki Tawi la Mwanza, Godfrey Banza amesema,benki hiyo kila mwaka utumia Wiki ya Huduma kwa Wateja kuwashukuru wateja kwa kuendelea kufanya kazi na benki hiyo.

Amesema mbali na kuwashukuru, benki hiyo utumia wiki hiyo kufanya shughuli zinazogusa jamii moja kwa moja, ikiwemo huduma ya upimaji wa macho bure iliyotolewa mwaka huu kwa kushirikiana na Hospitali ya Dr. Agarwals, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango na thamani ya wateja.

“Kitendo hiki kinaonesha kwa kiasi gani sisi Mwanga Hakika Benki tumeweza kurejesha kwa wateja wetu. Pia tuliandaa vitu mbalimbali, ikiwemo kukata keki kwa kushirikiana na wateja wetu na chakula cha pamoja,”amesema Banza.

Banza amesema,huduma hiyo pia imesaidia kuwaondolea wateja gharama ambazo wangetumia kufika hospitalini, hivyo benki hiyo imechangia moja kwa moja katika afya ya wateja wake, huku akisema mwitikio umekuwa mkubwa na watu wengi wamejitokeza kupata huduma hiyo.

Amesema benki hiyo imejipanga kwenda mbali zaidi kwa kusaidia hospitali zinazohitaji vifaa, huku pia ikipanga kushiriki katika shughuli za michezo, akisisitiza kuwa Mwanga Hakika Benki inaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na kurejesha kwa jamii.

Kwa upande wa huduma za kibenki, Banza amesema,benki hiyo sasa imeenea hapa nchini ambapo kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma kupitia Pesa Hakika App, ambayo inamwezesha mteja kupata huduma za benki akiwa mahali alipo.

Amesema katika kipindi cha takribani miezi mitatu tangu kuanzishwa kwa tawi la Mwanza, benki hiyo imefikia wateja 9,000, sawa na wastani wa wateja 3,000 kwa mwezi, huku lengo likiwa ni kuwafikia watu wengi zaidi kupitia huduma za kidijitali.

Amesema Wiki ya Huduma kwa Wateja imekuwa na mafanikio makubwa, hasa kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa benki hiyo kushiriki katika shughuli hizo Mwanza, ambapo imewapa fursa ya kuwafahamu wateja zaidi, kusikiliza mahitaji yao na kuwaelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo.

Aidha, amesema benki hiyo ina wataalamu wanaotoa elimu ya fedha na biashara kwa wateja wanaohitaji mikopo, ambapo kabla ya kuwapatia mikopo hupewa elimu na kuandaliwa ili fedha hizo zitumike kwa namna itakayozalisha matokeo chanya, huku benki ikiwa na ushuhuda wa wateja waliowahi kusaidiwa kuinuka kiuchumi.