October 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EWURA yawakumbusha wateja haki zao

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA),Kanda ya Ziwa imewataka watumiaji wa huduma za nishati na maji kuzifahamu haki zao, ikiwemo kuunganishiwa huduma ndani ya muda uliowekwa kwenye mikataba ya huduma kwa wateja na kupata fidia endapo mtoa huduma atashindwa kutimiza wajibu huo.

Akizungumza Oktoba 8,2026 katika Wiki ya Huduma kwa Wateja kupitia mahojiano maalumu Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira amesema,mamlaka hiyo inasimamia nishati ambayo inajumlisha sekta ndogo ya petroli, umeme na gesi asilia pia maji mijini,utoaji wa leseni, ubora wa huduma na bei.

Musira amesema,eneo linalohitaji elimu zaidi ni haki za wateja wanaopokea huduma, hasa haki zilizo kwenye mikataba hiyo . “Mfano moja ya haki ambayo tumekuwa tukiieleza hapa ni haki ya mteja kuunganishiwa huduma ndani ya muda ambao mtoa huduma ameusema kwenye mkataba wake,” amesema.

Musira amesema mteja ana haki ya kupata fidia endapo huduma haijatolewa ndani ya muda uliotajwa kwenye mkataba huku EWURA pia hushughulikia malalamiko kama bili za kubambikizwa, mafuta yasiyo safi au madhara yanayotokana na huduma ya umeme.

Amesema wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko hayo EWURA, ambayo hutoa maamuzi yenye nguvu sawa na uamuzi wa Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria na katika Wiki ya Huduma kwa Wateja katika banda la mamlaka hilo linapokea wastani wa zaidi ya wateja 30 kwa siku, wanaofika kupata elimu, kufahamu namna ya kupata leseni na kushughulikia changamoto mbalimbali.

Sanjari na hayo Musira amesema, EWURA imerahisisha masharti ya uwekezaji wa vituo vya mafuta vijijini, ambapo mwombaji hulipa sh.50,000 kwa maombi na sh.100,000 kwa leseni ya miaka mitano, tofauti na mijini ambapo maombi ni sh.500,000 na leseni sh milioni 1, huku akisitiza kuwa wanaofunga mifumo ya umeme kwenye majengo wanapaswa kuwa na leseni kutoka mamlaka hiyo.

Amesema changamoto nyingine ni watu kutoa huduma zinazodhibitiwa bila leseni, jambo ambalo ni kosa la jinai. Ametaja vishoka wanaofanya kazi za umeme bila leseni na uuzaji usio sahihi wa mitungi ya gesi na petroli kwenye chupa, akisema vitendo hivyo ni hatari kwa usalama wa watu na mali zao.

Musira amesema EWURA imehamishia huduma zake nyingi kwenye mfumo wa kidigitali, hivyo wateja wanaweza kuomba leseni, kuwasilisha malalamiko na kupata huduma nyingine kupitia tovuti bila kufika ofisini ambapo teknolojia imewezesha mamlaka hiyo kuwafikia wateja kwa urahisi na haraka.