January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwalimu, mwanafunzi wauwawa mkoani Mbeya

Na. Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MWALIMU wa Shule ya msingi Mbugani wilayani Chunya mkoani Mbeya aitwaye,Herieth Lupembe (37) na Mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya sekondari Isenyela Ivin Tatizo (15) wameuwawa kwa kushambuliwa na vitu butu kichwani wakiwa nyumbani kwao Kijiji cha Kiwanja wilayani hapa.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea Machi 31, 2024 majira ya saa 2:30 usiku wakati marehemu akiwa nyumbani kwake.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa katika nyumba hiyo alikuwepo marehemu na watoto wawili ambao ni Ivon Tatizo ambaye naye ni marehemu na Haris Barnaba Mtweve (06) Mwanafunzi wa darasa la kwanza shule ya msingi Ken Gold aliyejeruhiwa kwa kupigwa na kitu butu kichwani.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa, mtu huyo aliwavamia marehemu na kuanza kuwashambulia na baada ya kufanya hivyo alifunga milango kwa nje na kuondoka na funguo.

Chanzo cha tukio hili bado kinachunguzwa na majeruhi Haris anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na msako dhidi ya mtu au watu waliohusika.

Aidha ametoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa za mtu au watu waliohusika katika tukio hilo kutoa taarifa ili wakamatwe