April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwalimu akamatwa kwa wizi wa milioni 34

Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya

MWALIMU wa Shule ya Msingi Mwakareli, Joseph Shila (29) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za wizi fedha shilingi milioni 34 ambazo ni mali ya Mwalimu Mstaafu Gideon Mwalujobo (60) mkazi wa Mwakareli mkoani humo. 

Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema mtuhumiwa alikamatwa June 30 mwaka huu saa moja usiku katika Kata ya Mwakareli, Tarafa ya Busokelo, wilayani Rungwe. 

Amesema kuwa baada ya polisi kupata taarifa toka kwa msiri na kwamba mtuhumiwa alifanikiwa kuiba fedha hizo za mwalimu mwenzie  kupitia akaunti kwa kutumia NMB Mobile katika Tawi  la Mbalizi Road baada ya kupata namba ya siri ya Mwakujobo. 

Aidha Matei ameongeza kuwa Mwakujobo alikuwa ni walimu wa shule Moja na marafiki wa siku nyingi na mtuhumiwa. 

Amesema pia mtuhumiwa pia anajihusisha na uwakala wa kusajili laini za simu kwa kutumia mfumo wa kisasa wa alama za vidole ambapo aliweza kutengeneza laini ya simu kwa jina la Mhanga na kutokana na kuaminiana na mhanga pia alikuwa ana mpa kadi yake ya benki kwa ajili ya kumtolea fedha..

Katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa mtuhumiwa amekutwa na fedha taslimu Tshs. Milioni 20,780,000/=, Kadi ya Benki NMB, Simu tatu aina ya Tecno na laini mbili za simu. 

Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ulrich Matei ametoa wito kwa wananchi kuwa makini na kadi zao za benki ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatunza namba ya siri ili kujiepusha na matukio ya wizi.