Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BAADA ya bondia Hassan Mwakinyo kufanikiwa kutetea ubingwa wake wa Mabara wa uzito wa Super Welter wa WBF kwa kumchapa kwa ‘Technical Knock Out’ (TKO) ya raundi ya nne Jose Carlos Paz kutoka Argentina, bondia huyo amesema hatofanya makosa katika pambano lake lijalo la kuwania ubingwa wa dunia wa WBF.
Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Februari 2021 kuzichapa na bondia Lasha Gurguliani kutoka Georgia.
Akizungumza mara baada ya kutwaa ubingwa huo, Mwakinyo amesema kuwa, kila anapomaliza pambano moja basi hufanya mazoezi mara mbili zaidi ya alivyojiandaa awali hivyo wapenzi wa ngumi wasitarajio kuone kiwango alichokionesha dhidi ya Paz katika pambano lijalo.
“Baada ya kushinda pambano hili nimepata nafasi ya kucheza ubingwa wa WBF, nitashinda kwa mara nyingine tena kupitia kwa kocha wangu huyu huyu ambaye watu walikuwa kimbeza kuwa si kocha mzuri,” amesema Mwakinyo.
Hata hivyo bondia huyo ameweka wazi kuwa, ana imani ushindi wake dhidi ya Paz sasa utawafanya baadhi ya mabondia wenzake wa hapa nchini waliokuwa wakitaka pambano dhidi yake hawatorudia tena kumtaja.
“Mimi sio ‘boxer’ wa kufananisha na yeyote hapa nchini na nadhani kiwango nilichokionesha kimedhihirisha hilo kwani mara zote nawaambia mashabiki wangu kuwa mechi zinakuwa ngumu kulingana na ugumu na wapinzani na udhaifu wa elimu kwa makocha wetu hivyo wale waliokuwa wananitaja taja nadhani leo itakuwa mwisho wao kuongea kwani mimi ndio Tanzania One, ” amesema Mwakinyo
Katika pambano lake, Mwakinyo alionesha kiwango cha juu tofauti na ilivyokuwa katika mapambano yake mawili yaliyopita huku wakianza kushambuliana kwa kasi na Paz ambaye aye alionekana kuwa bora.
Mwakinyo alirudi tofauti katika raundi ya pili baada ya kugundua udhaifu wa mpinzanin wake na kuanza kumpiga ngumi za tumbo akitumia jabu ambazo zilionekana kumpa wakati mgumu mpinzani wake huku makonde aliyomchapa mfumulizo yakimdodhosha Paz lakini bado alikuwa na nguvu ya kuendelea kupambana.
Raundi ya tatu Paz naye alianza kujibu mashambulizi kwa Mwakinyo ambaye pia kwa bahati mbaya aliteleza na kuanguka lakini aliinuka na kuendelea na pambano ambalo lilikuwa kali zaidi raundi ya nne ambayo ilikuwa ya piga nikupige lakini uimara wa Mwakinyo ulimfanya kumpeleka tena chini mpinzani wake kwa ngumi kali ya tumbo.
Licha ya kitendo hicho lakini Paz aliendelea na pambano na Mwakinyo alimshambulia kwa makonde ya mfululizo jambo lililomfanya mwamuzi Edward Marshall kulisimamisha pambano na Mwakinyo kutwaa ubingwa.
Mbali na Mwakinyo, Mwanadada Fatuma Zarika kutoka Kenya amefanikiwa kutwaa ubingwa wa WBF (Kg 57) baada ya kumchapa Mzimbabwe Patience Mastara kwa pointi.
Pambano kati ya Hussein Itaba wa Tanzania dhidi ya Alex Kabungu kutoka DR Congo limemalizika kwa sare tofauti na ilivyotangazwa awali kuwa mshindi alikuwa ni Alex.
kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa na majaji ni kwamba pambano hilo limemalizika kwa sare kutokana na majaji wawili kuwapa pointi sawa mabondia hao huku mmoja tu ndiye aliyempa ushindi Alex .
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM