May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwaka 2022:

Samia aitoa Tanzania
kwenye siasa za giza

Na Mwandishi Wetu

WAKATI mwaka 2022 ukielekea ukingoni, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa kinara kwenye medani za siasa baada kuitoa Tanzania kwenye siasa za giza zilizodumu kwa takribani miaka sita.

Hiyo inadhihirishwa na kauli za wanasiasa waliokuwa wakieleza jinsi Rais Samia alivyotumia mwaka huu kurejesha mahusiano yaliyokuwa gizani baina ya wanasiasa na Serikali.

“Mwaka huu, umekuwa mwaka wa kihistoria katika medani za siasa, kutokana na Rais Samia kuamua kukaa na viongozi wa vyama vya siasa na kuzungumza nao ili kumaliza tofauti alizozikuta wakati akishika wadhifa huo baina na Serikali Awamu ya Tano na vyama vya siasa kwa miaka sita,” alisema Edward Aman mfuasi wa Tanzania Labour Party (TLP).

Aidha juhudi hizo za Rais Samia kuondoa taifa kwenye siasa za giza zinatambuliwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ambaye mwezi huu aliwaambia Watanzania waishio Marekani kwamba suala la maridhiano ni jambo la muhimu kwa maslahi ya Taifa.

Mbowe alisema katika kipindi cha miaka sita iliyopita Tanzania ilikuwa kwenye siasa za giza na utawala wa mabavu.

Alisema hiyo ilisababisha madhara makubwa kwa CHADEMA. “Kama ambavyo imeisharipotiwa mara kadhaa demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu vimekuwa kifungoni kwa miaka sita nchini, tumekuwa kwenye utawala wa kimabavu na CHADEMA tumekuwa mhanga mkubwa wa utawala huo,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema kwa sasa anaongoza CHADEMA katika mazungumzo na Serikali kuponya majeraha na kurudisha demokrasia na kuwa msimamo wao katika mazingumzo hayo umekuwa wa wazi.

Mbowe alikutana na Rais Samia mara ya kwanza Ikulu jijini Dar es Salaam, mara baada ya kuachiwa huru kufuatia yeye na wenzake watatu kufutiwa mashtaka ya uhujumu uchumi na ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili.

“ Kitu kikubwa tulichojadiliana ni kuwa Tanzania ni yetu sote na tunapaswa kufanya kazi pamoja, kuijenga, lakini hili linawezekana tu iwapo tutajenga uaminifu na kudai haki, pamoja na kuheshimiana. Hii itatusaidia kupata nafasi ya kuijenga nchi yetu,” alisema Rais Samia wakati akieleza kile walichokubaliana na Mbowe.

Mbowe alisema mazungumzo yake na Rais Samia, yalifungua milango ya kukishirikisha chama chake hicho kama Taasisi, ambapo hadi sasa mazungumzo kwa ajili ya maridhiano yanaendelea.

Hatua hii imekuwa ikipongezwa na wadau mbalimbali nchini na kuelezwa kama jitihada za Rais Samia kutaka mshikamo wa kitaifa, hasa ikizingatiwa kwamba kabla ya hapo alikuwa ameishakutana na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu jijini Brussel nchini Ubelgiji, Februari, mwaka huu.

“Tumekubaliana kuwa, njia nzuri ya kuwa na maridhiano ni wakati kuna haki.Tumepitia madhila mengi, hakuna haja ya kuyarudisha mara kwa mara, badala yake tunapaswa kusonga mbele na kuwa na siasa safi na kuiunga mkono Serikali, na tunatumai kuwa itatuunga mkono kwenye shughuli zetu ili kila mtu afurahi, “ alisema Mbowe mara baada ya mazungumzo yake na Rais Samia.

Aidha, Baraza la Vyama vya Siasa lilimpongeza Rais Samia kwa kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, huku likiahidi kuendesha siasa za nchi kwa njia ya kistaarabu na kuzingatia misingi ya amani na utulivu.

Mwenyekiti wa baraza hilo, Juma Ali Khatib alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara, visiwani Zanzibar.

“Tumefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuiongoza Tanzania kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utulivu wa kisiasa,” alisema.

Khatib alisema baraza hilo litaendelea kuishauri serikali njia sahihi za kuendesha siasa za kistaarabu zinazozingatia maslahi ya Taifa na wananchi.

Khatib alisema vyama vya siasa nchini vinaendelea kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria na kuishauri serikali akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye mlezi wa baraza hilo.

Alisema watahakikisha wanakuwa daraja la uhusiano mwema na serikali kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi ambao ndio wanaounda vyama vya siasa na kuona vyama vipo kwa maslahi ya taifa na sio kujenga chuki na serikali na vyombo vya dola,” alisema.