Na Mwandishi wetu,Timesmajira,Online
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2021 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.
Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za utabiri Dkt. Hamza Kabelwa amesema Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma).
Dkt Kabelwa amesema, Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2021 ukiwa na mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi. Aidha, Mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli.
Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kabelwa amesema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hali ambayo inaweza kuleta uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo kutokana na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Ameongezea Dkt. Kabelwa
More Stories
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla