May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mukatesi: Ndoa mbili katika umri wa miaka 20

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online

KATIKA Kata ya Kayenze, wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza kuna kisiwa kinachoitwa Bezi.

Bezi ni kisiwa lakini pia ni moja ya mitaa ndani ya Kata ya Kayenze. Kutoka katikati ya Jiji la Mwanza inaweza kumchukua mtu hadi saa 3 ili kufika katika kisiwa hiki ambacho ni maarufu kwa shughuli za uvuvi.

Nilipada gari (coaster) kutoka katikati ya Jiji la Mwanza mpaka Igombe, Kata ya Bugogwa kwa nauli ya Sh. 850/-, kisha kutoa Igombe hadi Kayenze kwa usafiri wa pikipiki unaogharimu kiasi Sh.3,000/- au gari dogo kwa nauli ya Sh.1,500/-.Kutoka makao makuu ya Kata ya Kayenze nilipanda kivuko (ferry) cha Mv. Ilemela na baada ya saa moja na dakika kama 15 hivi nilifika kisiwani Bezi.

Baada ya kushuka kwenye kivuko, nilitembea kuelekea upande wa kaskazini na kutumia kati ya dakika 15 hadi 20 hivi, nikafika ilipo ofisi ya serikali ya mtaa huo wa Kisiwa cha Bezi.

Nyuma ya ofisi hiyo ziko nyumba ambazo ni makazi ya watu, hivyo niliendelea kutembea na nilivuka kama nyumba tano ambazo zimeachana ubali wa meta kama mbili mbili (zimebanana), na nyumba ya sita ndicho kilikuwa kituo changu anamoishi mwenyeji wangu.

Huyu siyo mwingine bali ni Mukatesi Shukuru (siyo jina lake halisi) ambaye ameolewa na mmoja wavuvi katika kisiwa hiki, akiwa ni mume wake wa pili baada ya kuachana na wa kwanza ambako alizaa mtoto mmoja.

Maisha ya Mukatesi Simulizi ya binti huyu mwenye umri wa miaka 20 hivi sasa ni ndefu kwani katika kukua kwake alichkuliwa akiwa mdogo kwenda kuishi na walezi wake katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambako aliandikishwa darasa la kwanza na kuanza maisha ya shule.

Hata hivyo anaeleza kuwa maisha yake ya shule hayakuwa mazuri kutokana na mateso ambayo alikuwa akiyapata kutoka wa walezi wake ambao ni mama yake mkubwa na mumewe (baba mkubwa).

Mukatesi anaeleza kuwa alikuwa akitumikishwa kwa kufanyishwa kazi nyingi lakini alipewa chakula kidogo na wakati mwingine alishinda au kulala njaa pasipo kula kabisa.

“Ndugu zangu (watoto wa walezi wake) walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka shule walikuwa hawafanyi kazi yoyote, wao walipewa chakula cha kutosha na kupata muda wa kupumzika,” anaeleza Mukatesi na kuongeza kuwa“Kutokana na wingi wa kazi, kuna wakati nilishindwa kwenda shule kuhudhuria masomo kwa siku kadhaa na wakati mwingine wiki nzima ilipita, hivyo nilijikuta wakati nikienda nakuta wenzangu wamesonga mbele,”.

Anaeleza kuwa kutokana na mazingira hayo, aliamua kuacha shule, lakini aliendelea kukaa kwa walezi wake kwa muda mrefu huku mateso ya kufanyishwa kazi nyingi na kupewa chakula kidogo tofauti na watoto wa walezi wake yaliendelea.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Kazi, 2004, mtoto chini ya miaka 14 anayeendelea na masomo haruhusiwi kufanya kazi wakati na saa za shule na zaidi ya hapo haruhusiwi/hapaswi kufanya kazi kwa zaidi ya saa tatu kwa siku.

Mazingira yaliyosababisha Mukatesi kukatisha masomo na kuacha shule akiwa darasa la pili yalisababisha binti huyo kukosa haki ya msingi ya kuendelezwa ambayo inahusu maendeleo ya mtoto kiakili ikijumuisha elimu rasmi na isiyo rasmi, tamaduni,mila na desturi sahihi za jamii yake, kiroho kwa maana ya imani na vipaji.

Haki hiyo pamoja na nyingine za watoto zinalindwa katika mikataba mikubwa miwili ya haki za watoto, ambayo ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (CRC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990.

Tanzania imeridhia mikataba hiyo miwili ambayo inatoa wajibu kwa Serikali, wazazi, walezi na wanajamii kwa ujumla kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vyote vya ukatili na ubaguzi.

Katika kuwezesha utekelezaji wake Tanzania imetunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo inataja haki zote za msingi za mtoto kama zilivyoelezwa kwenye mikataba hiyo na kuweka bayana kwamba uamuzi wowote kuhusu mtoto lazima uzingatie maslahi yake kama yanavyotajwa kwenye sheria na kanuni zake.Mukatesi angeweza kupata haki yake ya elimu kama mamlaka zingesimamia Sheria ya Elimu Namba 25 ya 1978 ambayo inalinda haki ya mtoto ya kupatiwa elimu, ikieleza wazi kwamba elimu ya msingi ni ya lazima kwa watoto wote na itatolewa bure.

Kadhalika kanuni za utekelezaji wa sheria hiyo zinaweka bayana kwamba ni kosa kwa mzazi atakayeacha kumwandikisha shule mtoto mwenye umri wa kwenda shule na pia ni kosa kwa mzazi anayeshindwa kumsimamia mtoto wake mpaka kuhitimu darasa la saba.Kwa mujibu wa sheria hiyo na kanuni zake, utoro ni kosa la jinai na hivyo mtoto mtoro au mzazi ambaye anasababisha mtoto wake awe mtoro wote wanaweza kushitakiwa kwa kosa la jinai.Kutoroka na kufanya kazi za ndaniMukatesi anaeleza kuwa kuacha shule hakukusaidia kupunguza mateso na karaha alizokua anapata.

“Nilikuwa napika chakula lakini wakati wa kula natumwa sehemu na wao wanaendelea kula pamoja na watoto wao,nikirudi nakuta chakula kimeisha hivyo nalazimika kushinda njaa, ndipo nilipoamua kukimbilia Mwanza ambako nilikwenda kufanya kazi za ndani,”anaeleza Mukatesi.

Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2021 iliyotolewa na Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) inabainisha kuwa ukatili wa kimwili na kisaikolojia dhidi ya watoto ni miongoni mwa matukio ambayo yalibainika watoto kufanyiwa, yakishika nafasi ya pili nyuma ya ukatili wa kingono.

Katika utafiti uliofanywa na LHRC wanajamii walioshiriki waliwataja ndugu wa karibu au wanafamilia kama wafanyaji wakuu wa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 66 wakifuatiwa na wakina baba asilimia 47.

“Kupitia utafiti wa matukio yanayoripotiwa na vyombo vya habari na programu ya ufuatiliaji wa haki za binadamu, LHRC ilikusanya takribani matukio ya ukatili wa kimwili na kisaikolojia dhidi ya watoto,ambapo matukio hayo yaliripotiwa katika Mikoa ya Kagera, Rukwa, Mtwara, Ruvuma, Singida, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Geita, Shinyanga, Mbeya na Arusha,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Bila kutaka kuingia kwa undani jinsi alivyotoroka, Mukatesi anaeleza kuwa alifanya kazi za ndani kwa muda mrefu kidogo na alipochoka aliamua kurejea kwa wazazi wake wanaoishi eneo la Kijiweni wilayani Sengerema.

Ripoti ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto Tanzania wa mwaka 2014 iliyozinduliwa na Ofisi ya taifa ya takwimu (NBS), inabainisha kuwa asilimia 84.2 ya wafanyakazi wa ndani ni watoto wa kike huku asilimia 15.8 wakiwa ni watoto wakiume.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati ya miaka 5 hadi 17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi, sekta ya kilimo, misitu na uvuvi, huku wengi wao wakiwa ni wale wanaoishi vijijini.

Wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk. Albina Chuwa alibainisha kuwa utafiti huo unabainisha kuwa watoto wanafanya kazi zaidi katika sekta za kilimo, misitu na uvuvi ambazo zinaajiri asilimia 92.1 ya watoto wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Kazi, 2004, mtoto chini ya miaka 14 hapaswi kuajiriwa, isipokuwa mtoto mwenye umri huo kufanya kazi nyepesi tu, ambazo hazina madhara kwa afya na maendelo yake.

Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mtoto wa umri wa miaka 14 na zaidi anapokuwa likizo au baada ya kuhitimu elimu ya msingi au akiwa hasomi kwa sababu nyingine zinazokubalika kisheria, anaweza kuajiriwa kufanya kazi kwa kipindi kisichozidi saa 6 kwa siku, lakini asiruhusuiwe kufanya kazi kwa saa tatu mfululizo bila ya walau saa moja ya mapumziko.

Kuolewa na kuishi na mume;

Mukatesi anaeleza kuwa baada kwenda Sengerema kwa mama yake, huko ndipo alipokutana na mwanaume ambaye alimshawishi kuingia katika ndoa akiwa na umri wa miaka 16.

Hii ina maana kwamba binti huyu aliolewa akiwa bado mtoto na kuingia katika orodha ya walioigia katika ndoa za utotoni.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mtoto namba 21 ya 2009, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto pamoja na Sera ya Maendeleo ya Mtoto, mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane (18).Kwa mujibu wa Shirika la World Vision Tanzania ndoa za utotoni ni ndoa kwa mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18, huku likibainisha kuwa nchini Tanzania, takribani asilimia 31 ya watoto ya wa kike wameolewa wakiwa na umri chini ya huo.

“Hii ni idadi kubwa na inapaswa kukomeshwa ili watoto wa kike walindwe na kuendelea sawa na watoto wa kiume,ndoa za utotoni zinavunja haki za binadamu ambazo zinaelekeza kuwa ‘mtu ni lazima awe na umri wa mtu mzima pale anapoingia katika ndoa, kwa ridhaa yake,” inasomeka sehemu ya chapisho la taasisi hiyo.

Takwimu za Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya (TDHS), 2015-2016 zinaonyesha kuwa asilimia 36 ya mabinti wenye miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18.

Adha kwa mujibu wa TDHS wa mwaka 2010 mikoa yenye viwango vikubwa vya ueneaji wa ndoa za utotoni hapa nchini ni pamoja na Shinyanga asilimia 59, Tabora asilimia 58, Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.

Kwa mujibu wa wataalamu, viwango hivyo ni sawa na kusema kuwa kwa wastani, wasichana wawili kati ya watano huolewa kabla hawajatimiza umri wa miaka 18.

Mukatesi anaeleza kuwa “Baada ya kuolewa nilikaa takribani mwaka mzima nikapata ujauzito nikiwa na miaka 17 na kufanikiwa kujifungua mtoto wa kike ambaye kwa sasa ana miaka miwili na miezi kadhaa.”

Anaendelea kueleza kuwa “Tuliendelea kuishi na mume wangu, lakini kimsingi maisha yalikuwa magumu kwa sababu ya kipato chake kuwa kidogo hivyo kushindwa kumudu mahitaji muhimu ya mtoto na mimi pia.”

Mbali na hayo anaeleza kuwa mama yake mzazi alikuwa anaishi na baba yake wa kambo ambaye alifariki miezi michache baada ya yeye kujifungua licha ya kuwa baba yake mzazi yupo ila hafahamu alipo.

Mukatesi anaekeza kuwa hali ya ugumu wa maisha ilisababisha mumewe kuamua kumpeleka yeye na mtoto kwa wazazi wake (wakwe zake) hukohuko Sengerema, lakini huko pia hali ya maisha iliendelea kuwa ngumu hivyo wakaachana na mume wake.

Anaeleza kuwa baada ya kuachana na mumewe, aliondoka na kumuacha mtoto kwa bibi yake (mama mzazi wa mwanaume) na kukimbilia Kisiwa cha Bezi ambako sasa ameolewa na mwanaume mwingine.

Anaeleza kuwa kwa sasa maisha yake na huyo mume wake wa pili yana unafuu kwa sababu hana mtoto ambaye ana mahitaji kama ilivyokuwa mwanzo.Neno kwa mambintiMukatesi anaeleza kuwa pamoja na kwamba yeye alikwama kimasomo, lakini wasichana wanapaswa kuzingatia masomo na kujiepusha na vishawishi ili kutimiza ndoto zao hata kama shule zipo mbali.

“Mimi nilikuwa na ndoto za kuwa Daktari lakini nimeangukia katika ndoa na mimba za utotoni ambapo kwenye kulea mtoto kuna changamoto kwa sababu umri wangu ulikuwa mdogo na hali ya uchumi ilikuwa ngumu,”anaeleza Mukatesi.

Hata hivyo ameiomba serikali ijenge mazingira rafiki kwa watoto wa kike kuweza kutimiza ndoto zao na kuepuka kuingia kwenye ndoa za utotoni.

Anaekeza kuwa serikali ichukue hatua kuziba mianya yote ambayo inaweza kuchangia mtoto wa kike kupata vishawishi vitakavyofanya binti kuingia kwenye mapenzi akiwa na umri mdogo.Pamoja na kwamba hakuwa na maelezo marefu, Mukatesi anaweza kuwa anaungana na wale ambao wamekuwa wakitoa wito kwa Serikali kuufanyia kazi mkanganyiko wa kisheria hasa unaogusa umri wa kuolewa kwa mtoto wa kike.

Sheria ya Ndoa, Sura ya 29 ya mwaka 1971 kama ilivyorekebishwa mwaka 2019 ni Sheria kuu inayosimamia masuala ya ndoa nchini Tanzania ambayo inatajwa kuwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kuruhusu mazingira fulani ya ubaguzi wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.

Tamko lililotolewa na mashirika ya utetezi wa haki za binadamu wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia linasema kuna ukinzani wa kisheria kwani wakati Sheria ya mtoto ikimtafsiri mtoto kama mtu yoyote mwenye umri chini ya umri wa miaka 18, Sheria ya ndoa inaruhusu msichana chini ya umri wa miaka 18 kuolewa.

“Kwa misingi hiyo, Sheria inatoa mwanya kwa ndoa za utotoni,vile vile Sheria hii inakinzana na kanuni za adhabu ambayo imeanisha kwamba ni kosa la ubakaji kwa mtu yoyote kufanya ngono na mtoto chini ya umri wa miaka 18 isipokua kama ameolewa,” inasomeka sehemu ya tamko hilo.

Katika tamko hilo, wanaharakati wanaitaka Serikali kutekeleza hukumu ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania iliyothibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya ndoa ambavyo vinaruhusu mtoto kuolewa na umri wa miaka 15 kwa idhini ya wazazi na 14 kwa ruhusa ya mahakama ni vya kibaguzi dhidi ya mtoto wa kike na ni kinyume na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika kesi hiyo ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mahakama ya Rufani ilisema vifungu husika vinapaswa kurekebishwa ndani ya miezi 12 jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika.

Mara kwa mara Serikali imekua ikikiri kwamba kushindwa kubadili kifungu hicho ni kutokana na unyeti wa kitamaduni na wa kidini juu ya jambo hilo. Hivi karibuni Jaji Mstaafu Robert Makaramba wa Mahakamu Kuu ya Tanzania, alisema baada ya hukumu ya Mahakama ya Rufani katika kesi hiyo, umri wa kuolewa hauwezi kushushwa na taasisi yoyote ile.

“Hata kama Sheria ya Ndoa haijabadilishwa, lakini katika muktadha wa mamlaka ya mahakama, uamuzi wa Mahakama ya Rufani ni sheria tayari. Bunge linaweza kurekebisha mambo mengine katika sheria husika, lakini suala la umri ambalo limetolewa uamuzi na Mahakama ya Juu kabisa katika nchi yetu, haliwezi kubadilishwa nje ya mfumo wa kimahakama,” alisema Jaji Makaramba katika hafla ya uzinduzi wa machapisho ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).