Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
JESHI la Polisi Mkoa wa Songwe linamtafuta, Masumbula Nemson, Mkazi wa Kitongoji C katika kijiji cha Namkukwe, wilayani Songwe kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wa miezi mine baada ya ugomvi na mke wake.
Nemson anadaiwa kumuua mtoto wake huyo wa miezi minne, Blasto Nemson kwa kumpiga na fimbo kichwani upande wa kulia akiwa mgongoni mwa mama yake.
Ugomvi huo unaohusisha wivu wa mapenzi, unadaiwa kuibuka baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mkewe kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume mwingine.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya, Machi 9, mwaka huu akizungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Machi 8, 2024 majira ya saa 2:00 usiku na baada ya mtuhumiwa kufanya kitendo hicho alitoroka na kikimbilia kusikojulikana.
“Upelelezi unaoambatana na msako unaendelea kumtafuta mtuhumiwa,pindi akikamatwa atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,”amesema Kamanda Mallya.
Pia ameeleza kuwa katika tukio hilo, pia mama wa marehemu alijeruhiwa kichwani na mikono yake yote miwili wakati akijikinga na kumkinga mtoto wakiwa wanashambuliwa kwa fimbo na mtuhumiwa.
More Stories
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano