Judith Ferdinand,Mwanza
MKURUGENZI wa Shirika lisilo la kiserikali la Toner Foundation, Josephat Toner (40), Mkazi wa Ghana Wilayani Ilemela mkoani Mwanza, amefariki kwa ajili ya gari.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Muliro Muliro, ajali iliyosababisha kifo cha mwanaharakati huyo ilitokea juzi Apirli 12, mwaka huu saa 2:05 usiku.
Alisema ajali hiyo ilitokea katika Barabara ya Makongoro, eneo la Kifua Wazi Rocky Mall, Kata ya Kirumba, Wilaya ya Ilemela ikihusisha gari namba T.263 CZQ Toyota Haice ambayo ni daladala linalofanya safari zake kati ya Kisesa – Nyasaka Mzunguko, ilimgonga na kusababisa kifo chake.
Alisema gari hilo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Mwanasalaha. Kamanda Muliro alisema dereva huyo alimgonga mwanaharakati huyo wakati akitokea mjini kwenda Nyasaka.
“Baada ya tukio hilo dereva alitelekeza gari na kukimbia, jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na mmiliki wa gari hilo na wananchi kwa ujumla wanamtafuta ili akamatwe na hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake,”alisema Muliro.
Aliongeza kuwa, uchunguzi kuhusu ajali hiyo unakamilishwa huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure kusubiri uchunguzi wa daktari.
Alisema pindi uchunguzi utakapo kamilika mwili utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.
Alitoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu kuendelea kuwa makini na kufuata sheria wakati wanapotumia barabara.
Shirika la mwanaharakati huyo lilikuwa likijihusisha na uteteaji wa watu wenye Ualibino.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya