April 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtanzania aula Rwanda, Jesica aweka rekodi ya kibabe

Na Mwandishi Wetu

NYOTA wa zamani wa timu ya Taifa ya Kikapu ya Tanzania aliyewahi kuzitumia timu za Pazi, Savio Henry Mwinuka ameteuliwa na Shirikisho la mpira wa kikapu nchini Rwanda (FERWABA) kuwa kosa msaidizi wa timu ya Taifa ya Rwanda inayojiandaa kushiriki mashindano ya Afrika (Afrobasket) yanayotarajiwa kufanyika nchini Rwanda 2021.

Licha ya kuwa mchezaji mahiri pia amewahi kufundisha timu kama UDSM Outsiders ya Tanzania, Patriots ya Rwanda iliyofanikiwa kuchukua mfululizo ubingwa wa Rwanda na ubingwa wa kombe ka FIBA Africa kanda ya tano ambao kwa sasa wanashiriki Basketball Africa League (BAL).

Akimpongeza kwa uteuzi huo, rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa amesema, hadi anateuliwa, Mwinuka alikuwa ni kocha Mkuu wa timu ya REG inayomilikiwa na Shirika la Umeme la Rwanda.

Amesema, katika msafara ambao aliuongoza mwaka 2011 wa timu ya Taifa ya Tanzania kushiriki Mashindano ya FIBA kanda ya tano nchini Rwanda, Mwinuka alikuwa ni miongoni wa mwa wachezaji nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania na kwa kiasi kikubwa kuchangia safari yake ya mafanikio kwani aliporejea nchini licha ya kuendelea kucheza na kufundisha alijiendeleza zaidi na akashiriki mafunzo kadhaa ya ualimu wa kikapu yaliyoandaliwa na TBF na kuendeshwa na FIBA na kuwa mmoja wa makocha waliofanikisha kumuibua na kumsaidia sana mchezaji nyota wa NBA, Hasheem Thabeet.

“Kwa niaba ya Shirikisho na Watanzania wote tunampongeza sana Henry Mwinuka na kumtakia mafanikio makubwa zaidi katika majukumu yake hayo mapya,” amesema Magesa.

Rais huyo pia alimpongeza mchezaji Jesica Ngisaise wa timu ya wanawake ya JKT kwa kuingia katika historia ya wachezaji waliofunga pointi nyingi zaidi ya 100 duniani.

Jesica Ngisaise

Jesica alifanikiwa kufunga pointi 105 pekee yake katika mchezo kati ya JKT dhidi ya Ukonga Princess katika Ligi ya Kikapu ya wanawake (RBA) inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Jesica pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania na ameshiriki matukio na michezo mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwemo Senegal, Kenya, Afrika Kusini ambako alishiriki kambi Basketball Without Border 2018 na kufanikiwa kuchaguliwa katika timu ya nyota bora wa Afrika ya Wasichana na kucheza mchezo wa utangulizi kabla ya mchezo wa NBA uliofanyika Sun Arena, Pretoria, 2018.