January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtandao dawa za kulevya wakamatwa Dar

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

WATU saba wamekamatwa na Kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine, katika msako maalumu uliofanyika Jijini Dar es Salaam na Iringa, Desemba 5 hadi 23, Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema kati ya waliokamatwa wawili wana asili ya Asia, wengine ni watanzania.

Amesema, ukamataji wa dawa hizo umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya, ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia hapa nchini, tangu kuanzishwa kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya.

Hata hivyo amesema watuhumiwa hao ni miongoni mwa wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaofuatiliwa nchini na duniani kwa ujumla.

Lyimo amesema, wakati wa msako, dawa hizo zilikutwa zimefungwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai, huku akidai kuwa mbinu hiyo imekuwa ikitumika kwa lengo la kurahisisha usafirishaji na kukwepa kubainika.

“Wakati wa oparesheni hii, dawa hizo zilikutwa zimewekwa katika vifungashio vya kahawa na majani ya chai, ambapo kwa haraka mtu ukiona unaweza jua pengine ni kahawa au majani ya chai.

“Lakini ndani dawa za kulevya, na wanafanya hivi kwa kukwepa kubainika na kurahisisha usafirishaji,” amesema Lyimo.

Aidha, amesema dawa hizo endapo zingefanikiwa kuingia mtaani, zingeathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku, hivyo Mamlaka imeokoa kiasi hicho cha watu ambao wangeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.

Lyimo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka hiyo kwani mafanikio yake hutokana na wananchi wanaotoa taarifa dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

“Natoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mamlaka, kwani wao ndiyo wanaofanya sisi kufanikiwa kutokana na kupata taarifa kwa watu,”ameongeza Lyimo.

Mamlaka inaishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezeaha Mamlaka hiyo katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.