December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtaka:TOC wasaidieni wachezaji wanaichipukia wajitambue

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MKUU wa mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka ameiagiza Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) kuwasaidia wachezaji watanzania wanaochipukia ili waweze kujitambua na kupanga mikakati yao ya ushiriki wa mashindano ya kimataifa.

Mtaka amewapongeza TOC kutokana na kusaidia katika michezo, na
kuongeza kuwa jambo la msingi ni kuhakikisha wanavifuatilia vyama
hivyo ili viweze kufanya vizuri.
Akifungua  Mkutano Mkuu wa TOC jijini hapa  kwa kushirikisha wanachama wake mbalimbali,Mtaka amesema wanariadha wengi wa Tanzania hawajitambui,  hivyo wanahitaji msaada mkubwa kutoka kwa wakongwe ambao tayari walishashiriki katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo.
Amesema lengo la kufanya hivyo  ni kuona wanariadha wanafanya vitu vya maana na siyo kukimbilia  kwenda nje kushiriki mashindano ya riadha.
Amesema mchezaji anapoanza anahitaji kusonga mbele, lakini asonge
mbele kwa manufaa na sio kwenda tu ilimradi amekwenda nje.
Hata hivyo, amesema TOC bado inakazi kubwa ya kuhakikisha inawainua wachezaji wote ili waweze kuiwakilisha vizuri taifa katika mashindano mbalimbali.
Amesema wanahitaji kuona wachezaji wote wanafanya vitu vizuri ili
waweze kufika mbali katika michezo wanayofanya katika mashindano mbalimbali.
Naye Makamu Mwenyekiti wa TOC, Henry Tandau amesema wanamshkuru Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mtaka kutokana na kutoa sapoti kwa watu wa michezo.
Amesema Mtaka amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha michezo inasonga mbele hapa nchini.
Aidha amesema wanahitaji kuwa na uwanja ambao utakuwa unatumika kwa ajili ya ichezo mbalimbali ili kusaidia kuinua vipaji vya wanamichezo.