Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
SERIKALI kupitia Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, imewataka wananchi kuzingatia usalama wa vitambulisho vyao vya Taifa (NIDA), kwa kuhakikisha kila laini ya simu inasajiliwa kwa kutumia kitambulisho cha NIDA cha mmiliki halali na inabaki chini ya matumizi yake.
Msigwa ametoa kauli hiyo hilo mapema leo, Septemba 1, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Septemba ya Utambulisho, kuelekea Siku ya Utambulisho Duniani itakayoadhimishwa Septemba 16 mwaka huu.
Msigwa amesema baadhi ya wananchi wamekuwa na tabia ya kukabidhi vitambulisho vyao vya Taifa kwa ndugu, marafiki au watu wengine kwa ajili ya kusajili laini za simu, bila kufahamu kuwa wanaweza kuwajibika kisheria endapo laini hizo zitatumika katika matukio ya uhalifu.
Amesema kumekuwa na baadhi ya wananchi wanaotumia vitambulisho vya NIDA vya watu wengine kusajili laini za simu, hususan kwa ajili ya watu ambao hawana sifa za kusajili laini hizo kwa majina yao.
“Baadhi ya wananchi wamekuwa wakikabidhi vitambulisho vyao kwa ndugu au marafiki kwa nia ya kuwasaidia, bila kufahamu matumizi ambayo mhusika atayafanya baada ya kusajili laini hiyo,” amesema.

Kwa mujibu wa Msigwa, katika baadhi ya matukio, watu waliokumbwa na matatizo ya kisheria kutokana na matumizi ya laini za simu wamebainika kuwa laini hizo zilisajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya NIDA vya watu wengine.
Amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kumkabidhi mtu mwingine kitambulisho chao cha NIDA, kwa kuwa endapo kitambulisho hicho kitatumika katika tukio lenye madhara kwa jamii, mwenye kitambulisho anaweza kuwajibika kisheria.
“Kitambulisho chako cha NIDA ni cha kwako wewe. Laini yako ya simu ni mali yako wewe. Sajili laini yako ya simu kwa kitambulisho chako na laini hiyo ibakie kwako,” amesema.
Aidha, amesema hata kama mtu atadai hakuhusika na tukio lililofanywa kwa kutumia laini iliyosajiliwa kwa kitambulisho chake, na kwamba alikikabidhi kitambulisho hicho kwa mtu mwingine, suala hilo linaweza kumweka katika mazingira ya kuwajibika kisheria.

More Stories
Fahari ya Z’bar 2026 kuwakutanisha wazalishaji zaidi ya 300
Rais Mwinyi azitaka nchi za NAM kuunganisha sauti
Salome:Wizara ya Nishati inajukumu kutoa umeme wa uhakika