May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa TCCP, mashine ya mammografia, kupunguza makali ya saratani nchini

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

MRADI mtambuka wa saratani Tanzania (TCCP) pamoja na mashine ya uchunguzi wa saratani ya matiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando umezinduliwa ikiwa ni njia moja ya kupambana na ugonjwa wa saratani nchini.

Huku Waganga Wakuu wa Mikoa na wa Halmashauri wakitakiwa kupitia mipango yao na bajeti zao kutenga fedha kwa ajili ya kufanya uhamasishaji kwa jamii juu ya masuala ya saratani.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo na mashine hiyo iliofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Meneja Miradi wa TCCP, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan Tanzania Dkt. Harrison Chuwa amesema, mradi huo wa miaka minne umegharimu kiasi cha fedha za Kitanzania bilioni 32 (Euro milioni 13.3) huku mashine hiyo ya uchunguzi wa saratani ya matiti ikigharimu kiasi cha milioni 800.

Unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFP) na The Aga Khan Foundation (AFK) ambao lengo lake likiwa ni kupunguza magonjwa na vifo vya saratani katika mikoa inayolengwa ya Tanzania ambayo Dar es Salaam na Mwanza.

Dkt. Chuwa amesema utekelezaji wa TCCP ulianza Januari 2020 na inakadiriwa kusaidia vituo 100 vya afya vya umma vya Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza, pamoja na zahanati na vituo vya matibabu vya AKHST, Taasisi ya saratani ya Ocean Road na kituo cha matibabu cha Bugando ikijumuisha mashine ya mammografia ambayo wamezindua jana.

Amesema mradi unatumia mbinu kabambe ya kukabiliana na saratani, kushirikisha jamii na kujenga uwezo kwa wahudumu wa afya ya jamii zaidi ya 400 na kuongeza hamasa kwa kuchapa na kusambaza zaidi ya vitabu 3000 na 5000 vifaa vya habari, mawasiliano na elimu.

“Mashine hii mpya ya hali ya juu ya mammografia katika Hospitali ya Bugando ni ya kwanza ya aina yake katika ukanda wa ziwa na inatarajiwa kuhudumia idadi ya karibu watu milioni 12 katika uchunguzi wa wanawake na kushughulikia na saratani ya matiti katika hatua ya awali,”amesema Dkt.Chuwa.

Ambapo amesema zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani wanaokwenda kutibiwa katika taasisi ya saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam wanatoka Kanda ya Ziwa,hivyo kusimikwa kwa mashine hiyo ambayo inauwezo wa kupima wagonjwa 20-25 kwa siku,kutapunguza msongamano wa wagonjwa wa saratani katika taasisi hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR-TAMISEMI,Dkt.Ntuli Kapologwe amesema,Saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza na kusababisha vifo vya watu wengi ulimwenguni ambapo kwa mwaka wa 2021 nchini hapa jumla ya watanzania takribani 42,000 waligundulika na saratani.

Dkt.Kapologwe amesema mwitikio wa jamii katika kupima saratani ni mdogo,hivyo amewataka Waganga Wakuu wa mikoa na wa Halmashauri kupitia mipango yao na bajeti zao kutenga fedha kwa ajili ya kufanya uhamasishaji kwa jamii juu ya masuala ya saratani.

Amepongeza mradi huo wa kusaidia juhudi za serikali katika kupunguza maradhi ya saratani na vifo kwa jamii.

“Serikali pekee haiwezi kumaliza changamoto ya ongezeko la saratani hivyo tunaipongeza TCCP kwa ubunifu wao wa kuonesha mafanikio ya ushirikiano wa sekta ya umma katika kudhibiti saratani nchini,”amesema Dkt.Kapologwe.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,Dkt.Fabian Massaga, amesema wamezindua mashine hiyo ya kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti.

Hivyo amewahimiza wananchi wa Kanda ya Ziwa kutumia fursa hiyo kupima saratani kwani ikiwa katika hatua za awali inaweza kutibika lakini ikichelewa matibabu yake yanakuwa ni makubwa zaidi.

Meneja Miradi wa TCCP, Mkurugenzi wa Tiba kutoka Taasisi ya Huduma za afya Aga Khan Tanzania Dkt. Harrison Chuwa, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando. Picha na Judith Ferdinand
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR-TAMISEMI,Dkt.Ntuli Kapologwe, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu,katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa TCCP na usimikwaji wa mashine ya kufanyia uchunguzi wa saratani ya matiti katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, iliofanyika katika hospitali hiyo mkoani Mwanza. Picha na Judith Ferdinand
Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR-TAMISEMI,Dkt.Ntuli Kapologwe, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa mashine ya uchunguzi wa saratani ya matiti ,katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa TCCP na usimikwaji wa mashine ya kufanyia uchunguzi wa saratani ya matiti katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, iliofanyika katika hospitali hiyo mkoani Mwanza. Picha na Judith Ferdinand
Muonekano wa mashine ya uchunguzi wa saratani ya matiti iliyozinduliwa jana na Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe OR-TAMISEMI,Dkt.Ntuli Kapologwe kwa niaba ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando. Picha Judith Ferdinand.