January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa maji ulivyorudisha matumaini mapya kwa wananchi waishio mpaka wa Rusumo

Na Penina Malundo, timesmajira

WANANCHI waishio kijiji cha Rusumo wilayani Ng’ara Mkoani Kagera moja ya changamoto waliyokuwa wanakumbana nayo ni pamoja na ukosefu wa maji safi na salama ya kunywa hali ambayo ilikuwa inahatarisha afya zao.

Vitongoji ambavyo vimekumbwa na adha hiyo ni pamoja na Nyakahanga ,Rusumo,Katosa,Mwibumba na Kahaza ambao wamekuwa wakitembea umbali wa kilomita 5 kufata maji katika mto Akagera na Ruvuvu.

Hali hii imewasumbua muda mrefu wananchi hao ambao walikuwa wanapata shida ya maji kwa kununua sh.1000 kwa vitongoji vya mbali na vile vya karibu kama Kahaza,ilikuwa inawagharimu hadi kiasi cha Sh. 500 kwa dumu la lita 10.

Kwa gharama hii wananchi hao walikuwa wanatumia kiasi cha sh. 30000 hadi 15000 kwa siku 30 wakinunua maji dumu moja huku wakinunua madumu mawili walikuwa wanafikisha hadi 60,000 kwa hadi 30,000 mwezi.

Saraphina Ibrahimu(33)Mfanyabiashara na Mkazi wa Kijiji cha Rusumo ,anaelezea namna walivyoangaika kupata maji safi na salama katika kijiji chao hali iliyowafanya wengi wao kutumia maji ya mto bila kutibiwa.

Anasema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakipata shida hiyo kwa muda mrefu hali iliyowafanya kuwa hatarini kupata magonjwa ya tumbo na wengine kuharisha kutokana na kutumia maji ambayo sio salama.

”Upatikanaji wa maji katika kijiji chao kwa sasa umeweza kurudisha furaha kwao kwani hali ilikuwa mbaya kiafya na kiuchumi.

Anasema miaka ya nyuma wakazi wa kijiji hicho walikuwa hatarini kupata magonjwa mbalimbali hususani ya tumbo kutokana na kutumia maji ambayo si salama ya mto Ruvuvu na Akagera.

”Upatikanaji wa maji safi na salama kwa sasa umetufurahisha wakazi wa Rusumo na vitongoji vyake kwani tulikuwa na adha kubwa sana miaka ya nyuma baada ya mradi huu kufika hapa mpakani kwetu tunashukuru maji masafi na salama sasa lakini kwa sasa yanapatikana kwa wingi,kaya nyingi wananufaika na wafanyabiashara nao wananufaika,”anasema na kuongeza

”Hali ilikuwa mbaya kifamilia na ngumu watu walikuwa wanatumia maji ya mto Akagera ambayo kiafya yalikuwa sio mazuri,huku kwa watu waliokuwa wanaishi mbali na mto walikuwa wanatumia fedha nyingi kununulia maji,”anasema.

Saraphina anasema walikuwa wanatumia gharama kubwa ambayo wangeweza kutumia katika matumizi mengine ikiwemo kununulia vyakula.”lakini kwa sasa tunafurahi sana,tunashukuru Wakala wa Mpango wa Bonde la Mto Nile (Nile Basin Initiative NELSAP) na Serikali kwa hatua hii ya maji kuwepo muda wote ni sisi kujikadilia tu,”anasisitiza.

Aidha anasema kwa upande wa wafanyabiashara katika eneo hilo,walikuwa wanaumizwa ikiwemo wale wa mama ntilie,Saloon na waosha magari kwa kununua maji kwa gharama kubwa.”Mimi ninafanya mama ntilie nilikuwa natumia maji ya sh. 15000 hadi 20000 kwa siku ambapo kwa sasa natumia kiasi cha sh. 3000 hadi 5000,”anasema.

Saraphina anasema ni kiasi kikubwa wameweza kupunguza gharama katika matumizi ya maji ambayo yalikuwa yanawaumiza kwa kutoa fedha nyingi za kununua maji na maji yenyewe ni yale yanayotoka mtoni ambayo hayajatibiwa.

”Biashara inaenda kuwa nzuri kutokana na maji kupatikana watu wenye carwash ,mama ntilie,majumbani kile kipato tulichotenga kwaajili ya kununua maji,sasa tunaenda kutumia kwa mambo mengine,”anasema.

Innocent Magai Mkazi wa rusumo anaishukuru NELSAP na uongozi wa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaangalia wananchi wa rusumo kwa changamoto iliyowatesa miaka mingi ya maji kwa sasa hatua waliofikia ni nzuri kupitia mradi wa Rusumo Electronic Power.

Anasema Kijiji cha rusumo sasa vitongoji vyote vinapata maji kwa wakati ambapo mwanzo walikuwa wanapata kwa mgao na maeneo mengine yalikuwa hayapati kabisa maji.

Anasema ambapo dumu moja lilikuwa linauzwa 1000 kwa pikipiki ila kwa sasa wananunua dumu moja kwa kiasi cha sh. 50 kwa vituo vya maji.

”Tunashukuru Nelsap kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wa Rusumo wanapata maji safi na salama,ambapo sasa hivi mradi huu umekabidhiwa Ruwasa hivyo tutazidi kuutunza na kuhakikisha jamii inapata huduma stahiki kwa wakati,”anasema.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maji kijiji cha Rusumo mkoa wa Ng’ara,Ntiba Bilawa anasema miaka mitatu hadi miwili ya nyuma wamekuwa wahanga wakubwa wa utafutaji wa maji safi na salama katika eneo lao.

Amesema wamekuwa wakichota maji katika chanzo chao cha maji cha Mto Ruvuvu au Akagera ambapo walikuwa wanakumbana na vikwazo mbalimbali pindi wanaenda kuchota maji ikiwemo umbali mrefu wa uchotaji maji kutoka katika vitongoji hadi kwenye mtoni pamoja na kuliwa na wanyama.

Bilawa anasema ni kilomita tano walikuwa wanafata maji katika mto huo,ambapo kwa sasa familia nyingi zinapata maji kutoka mita 300 hadi 400 kwa maeneo yao wanayoishi.

”Baada ya kukabidhiwa mradi huu kwa kijiji chetu,tunashukuru mabomba yamewafikia watu moja kwa moja na hata katika shule za msingi ambazo awali watoto wetu walikuwa wanabeba maji ya vidumu kutoka mtoni na kwenda nayo shuleni,”anasema.

Anasema kuna umuhimu mkubwa wa uwepo wa miradi kama hiyo katika mazingira ya wananchi kwani inakuza uchumi kwa eneo husika mfano fedha tulizokuwa tunatumia kununua maji sasa tunaweza kulipia ada za watoto.

”Tunahaidi kuitunza sana miradi hii wito kwa serikali kuendelea kutusaidia pale tulipokuwa hatujafika, Nelsap waendelee kutusaidia na wawasaidie wengine ambao wanaenda kutekeleza miradi yao kama hii,”anasema.

Anasema mradi huo wa maji safi na salama, hadi sasa umewafikia watu 4000 na vituo 18 ambapo malengo yao ni kufikia watu 83000 kwa mwishoni mwa mwaka 2024 ambao wote watakuwa wamefikiwa.

Naye Msimamizi Mkuu wa Masuala ya Mazingira kwa mradi wa RUSUMO katika upande wa Miradi ya Kijamii (LADP),Hamdun Mansur anasema mradi huo wa maendeleo ni wa phase 11 ambapo umegharamia kiasi cha sh. 3,047,641,964.59 kwaajili ya wananchi wa kijiji hicho kupata maji safi na salama.

Anasema NELSAP iliona ni vema kuwapatia mradi huo wa maji kwani hapo awali watu wa maeneo hayo walionekana kuwa na shida sana ya kufata maji mtoni.

”Dhumuni kubwa la mradi huo ni kuwapa maji safi wananchi wa Rusumo ambao walitoa ardhi zao kuendeleza mradi huo wa Umeme,mbali na kuwalipa fidia ya kawaida kwa maeneo tuliyoyachukua na kulipa fidia ya nyumba zilizopata dosari lakini tuliona tuendeleze na miradi mingine ya kimaendeleo kwa wananchi hawa,”anasema.

Akizungumzia namna ya maji hayo wanavyoyaandaa na kuwafikia ananchi wa kijiji hicho cha Rusumo,Mansur anasema maji hayo wanayachukua kutoka mto ruvuvu ambayo yanapumpiwa kwenye matanki yao na kuyaweka dawa kwaajili ya kuua vidudu na kupelekwa katika Tanki la Juu ambalo linawafikia wananchi moja kwa moja.

Anasema kabla ya mradi huu hali ilikuwa sio nzuri kwani wananchi walikuwa wanatumia maji ya mto Ruvuvu au Mto Akagera ambayo yalikuwa hayajatayarishwa vizuri.

Mansur anasema kila nchi ziliweza kupata fedha za mpango wa maendeleo kwa awamu mbili tofauti (LADP) ni mpango unaolenga kuchechemua shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kujenga miundombinu mbalimbali iliyolenga kuboresha maisha ya wakazi wa rusumo.

“Kulikuwa na mradi wa maji unaohusisha vijiji vinne katika awamu ya kwanza ya Miradi ya Kijamii (LADP Phase 1),tuliuboresha na watu walikuwa wanapata maji kwa mgao lakini baada ya kuona umuhimu wa maji safi katika eneo hili tuliona katika Phase 11 ya mradi tuendelee kuboresha mazingira ya maji kwa maeneo ya karibu,”anasema na kuongeza

”Na maji haya yanatoka nchini Burundi na Rwanda,ambapo Kampuni ya Rusumo Power kwa kushirikiana na Serikali tatu Tanzania,Rwanda na Burundi zinaangalia namna gani wanaweza kuwa na mpango mzuri katika nchi hizo kushiriki kutunza mazingira katika maeneo yao ili maji yaweze kupatikana kwa wingi na yasiwe na madhara ambayo yataharibu mradi wa kufua umeme ,”anasema.

Anasema miradi hiyo ya maendeleo inatekelezwa na wilaya husika ambapo nchi yenyewe inakuwa inachagua ambapo kwa Tanzania ilichagua wilaya ya Ng’ara kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.

”Matumaini ya wakazi wa rusumo ya kuona mradi wa benki ya dunia ulioanzishwa mwaka 2017 pamoja na ujenzi wa bwawa la kufua umeme la maporomoko ya rusumo kuwa suluhisho la changamoto za maji wilayani humo,”anasema na kuongeza

”Mradi huu wa kufua umeme wa maporomoko ya Rusumo ulizinduliwa na program ya NELSAP unatazamiwa kuzinufaisha nchi tatu ambazo ni Rwanda,Tanzania na Burundi kwenye mpaka wao wa pamoja,”anasema.

Wakazi wa Rusumo,Tanzania,Kirehe Rwanda na Muyinga Burundi sehemu ambazo mradi huu unatekelezwa wanasema wamefaidika na mradi huu kwa asilimia kubwa.