Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online
SERIKALI imewataka viongozi wa taasisi zinazohusika na mradi wa kimkakati wa Magadi Soda, ulioko Engaruka wilayani Monduli Mkoa wa Arusha washirikiane ili mradi huo uanze kutekelezwa kwa wakati.
Mradi huo unaotarajiwa kuongeza ajira, malighafi za viwandani, kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Hayo yamebainishwa Desemba 21,mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah, akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandubya na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, walipotembelea mradi huo.
Ambapo lengo la kutembelea mradi huo ni kuona utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali ili uanze rasmi hivi karibuni.
Akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika mradi huo, Katibu Mkuu Dkt Abdallah amesema, ziara ya Makatibu Wakuu katika kuutembelea mradi huo ni ishara tosha kuwa Serikali imedhamiria utekelezaji wake uanze mara moja.
“Ziara hii imeshirikisha Wizara tatu na jumla ya taasisi nne na itafanya kazi kwa kushirikiana na vijiji vinne katika kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mradi na kuanza kutekelezwa ni dhahiri kuwa utasaidia kuboresha maisha ya wakazi wa Engaruka na Taifa kwa ujumla, kuongeza mapato kwa Serikali na ipo tayari kuhakikisha utekelezaji wake unaanza mara moja,’’ amesema Dkt. Abdallah.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amebainisha kuwa, kuanza kuchimbwa kwa madini ya magadi soda nchini kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, ambacho kimekuwa kikitumika kuagiza kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya malighafi hiyo viwandani.
“Sisi kama wasimamizi wa sekta ya madini nchini tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa magadi soda ni madini muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa viwanda vingi hapa nchini kwa kuwa yanatumika kama malighafi na tuna viwanda ambavyo tayari vinategemea malighafi hii muhimu,” amefafanua Mahimbali.
Katika hatua nyingine, Mahimbali amewataka wakazi wa Engaruka na watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza pale ambapo mradi huo utakapoanza kutekelezwa wake.
Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dkt. Nicolaus Shombe, amesema kuwa NDC kama mwekezaji kwa niaba ya Serikali, tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wake ikiwemo kufanyika kwa upembuzi yakinifu na tathmini ya mazingira.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Mwl. Happyness Laizer na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli, Muhsin Kassim, wamesema wapo tayari kupokea mradi huo huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa zitakazopatikana wakati wa utekelezwaji wa mradi huo.
Mradi wa magadi soda wa Engaruka ni moja kati ya miradi kumi na saba ya kimkakati ya Serikali ambao upo chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao unaelezwa kuwa utekelezwaji wake utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi kwa Taifa kwa kuwa utasaidia katika kutoa malighafi mbalimbali za Magadi soda kwa viwanda ndani na nje ya nchi, kutoa ajira 1000 za moja kwa moja kwa wananachi ambapo uwekezaji wake unatarajia kugharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 400.
More Stories
CPA.Makalla :CCM kutumia 4R za Rais Samia katika uchaguzi Serikali za Mitaa
CCM kutumia 4R za Samia Uchaguzi Serikali za Mitaa
Dkt. Mpango awasilisha salam za Rais Samia mazisha Baba yake mzazi, Gavana Tutuba