December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MPC,yang’ara tuzo za heshima Eagle Entertainment 2023

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Sengerema

Katika kutambua mchango wa waandishi wa habari kwenye jamii kampuni ya Eagle Entertainment inayojishughulisha na burudani imetoa tuzo ya heshima kwa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC) kwa mwaka 2023.

Akipokea tuzo kwa niaba ya Mwenyekiti wa MPC Edwin Soko, Judith Ferdinand katika hafla ya usiku wa tuzo uliofanyika Desemba 25,2023 usiku wa sikukuu ya Krismasi iliofanyika wilayani Sengerema mkoani Mwanza ameishukuru kampuni hiyo kwa kutambua mchango wa MPC kwa jamii na kuona inastahili tuzo hiyo.

“Wametuheshimisha MPC kwa tuzo hii kwa kuona tunastahili hivyo tunaahidi kuwapa ushirikiano na kuwa bega kwa bega kuhakikisha tunaitangaza Wilaya ya Sengerema na Mkoa wa Mwanza ili kuvutia wawekezaji na kukuza maendeleo ya taifa kwa ujumla,” ameeleza Ferdinand.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Eagle Entertainment na muaandaji wa tuzo hizo Hassan Kuku ameeleza kuwa MPC imekuwa ikiwasaidia waandishi wa habari kufanya kazi zao ambazo zina mchango mkubwa katika jamii.

Kuku ameeleza kuwa wameamua kutoa tuzo za heshima kwa taasisi na watu mbalimbali katika kutambua mchango wao kwa jamii ambapo mbali na MPC kupewa tuzo hizo pia taasisi nyingine ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na na Rushwa Tanzania(TAKUKURU) ambao wamekuwa na mchango katika jamii ya kuhakikisha wanakomesha suala la rushwa nchini ambayo ni adui wa maendeleo ya taifa.

Nyingine ni Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) ambayo imekuwa na mchango mkubwa za kuhakikisha wanatokomeza dawa za kulevya nchini kwani zina athari kubwa kwa vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.

Aidha kundi jingine lillilopatiwa tuzo za heshima ni shule ya sekondari Sengerema kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha sita pamoja na msaani wa vichekesho Brother K na msanii wa mziki H.baba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele, waandishi wa habari ni muhimu hivyo kupokea tuzo inawasaidia kuhamasika kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani bila waandishi wa habari Halmashauri inakuwa bubu na serikali inakuwa bubu.