May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa ataka vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amewataka vijana wote wa Mkoa huo kuchangamkia fursa mbalimbali za kuwaingizia kipato ili kujikwamua kiuchumi.

Ametoa rai hiyo juzi alipokuwa akizindua kampeni ya ‘Kijana Zungumza na Mkuu wa Mkoa” yenye lengo la kuwapa mbinu za kutumia fursa za kiuchumi zilizoko mbele yao iliyohudhuriwa na mamia ya vijana wa Mkoa huo.

RC alisisitiza kuwa vijana wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi ila wengi wao wanasubiri ajira tu huku kukiwa na fursa lukuki za kujiajiri.

Alibainisha kuwa wameanzisha Kampeni hiyo ili kuondoa kasumba ya kusubiri ajira za serikali au taasisi binafsi pekee na kutumia muda mwingi kulalamika wakati fursa za kujiajiri zipo nyingi.

Alifafanua baadhi ya fursa zilizopo kuwa ni uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.

Aliongeza kuwa fursa hizi hazihitaji nguvu kubwa ya uanzishwaji na kama watahitaji mtaji, serikali imeweka utaratibu wa kuwezesha makundi ya kijamii kupitia mikopo nafuu isiyo na riba ya asilimia 10.

Balozi Batilda alieleza dhamira yake kuwa ni kuona vijana wote wa Mkoa huo wakianzisha shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato ili kujiepusha na tabia zisizofaa.

‘Nataka ndani ya miezi mitatu mabadiliko yaanze kuonekana kwa vijana na jamii kwa ujumla kupitia kampeni hiyo’, alisema. 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Viva Promotion inayojishughulisha na uchapishaji, Sylvester Geneli alisema Kampeni hii ni fursa muhimu sana kwa kila kijana kuamua hatma ya maisha yake kwa kuanzisha mradi wa kiuchumi.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Madam Vai Investment, Vailet Lusana, alieleza kuwa yeye ni mfano wa kuigwa kwani licha ya kuajiriwa ameanzisha kampuni yake ambayo inamlipa zaidi kuliko hata ajira aliyonayo.

Mkuu wa MKoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Salha Burian (wa tatu kushoto) akiwa na Viongozi mbalimbali wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua hivi karibuni katika moja ya mikutano yake ya kuhamasisha shughuli za maendeleo, Picha na Allan Vicent.