May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa akagua eneo lililoharibiwa na mafuriko Kimange


Na Mwandishi Wetu

Mkuu wa Mkoa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge ametembeleaeneo la ujenzi wa kalavati lililomomonyoka katika barabara ya Segera-Chalinze eneo la Kimange na kuwataka madereva wa magari kufuata maelekezo ya Askari wa Usalama barabarani mara wafikapo kwenye eneo hilo.

Mvua kubwa iliyonyesha Jumamosi iliyopita, ilimomonyoa kingo ya barabara upana wa mita 60 na kuacha eneo la mita 1;30 ya njia kuwa salama na ambayo ndiyo inatumika.

Mhe. Kunenge amesema mara baada ya hitilafu hiyo, serikali sikifu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia wahandisi wa TANROADS walianza kazi mara moja ya kukarabati eneo hilo kwa kumwaga zege na kuweka makalavati mengine.

“Tumekuwa hapa tangu siku ya kwanza ili kuhakikisha kazi hii inakamilika ili wananchi waendelee na shughuli zao za kujenga uchumi.

“Upande unaotumika ni upande mmoja na hivyo magari yanapita taratibu hivyo kutakuwa na uwingi wa magari niwaombe ukiambiwa subiri wenzako wa upande mmoja wapiti subiri.” Alisema.

Alisema wataalamu wa TANROADS wamemuhakikishia kuwa kazi hiyo inatarajiwa kukamilika leo ingawa itahitajika kiasi cha siku saba ili zege lililowekwa liweze kushikamana vizuri.

Aliwaasa madereva kuwa makini  katika kipindi hiki cha mvua za masika nchini, wanapoona barabara imefunikwa na maji wasijaribu kupita kwani ni hatari.

Mkuu wa Mkoa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge (kushoto) akizunguzma mara baada ya kutembelea eneo hilo leo Aprili 17, 2023