April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa ahimiza ulinzi miundombinu ya umeme

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela  amewaasa wananchi wa mkoa huo ambao maeneo ya vijiji vyao yamepitiwa na mradi wa kusafirisha umeme unao unganisha nchi za Tanzania na Kenya, kuhifadhi na kulinda miundombinu ya umeme iliyo pita katika maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela akiambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha alipo tembelea machimbo ya mchanga katika Kata ya Lengijave kuona uharibifu unaofanywa katika miundombinu ya umeme. Na Mpigapicha Wetu

Mongela ameyasema hayo alipo tembelea eneo la machimbo ya mchanga yaliyopo katika Kata ya Lengijave, Wilaya ya Arumeru ili kujionea athari za uchimbaji mchanga ambazo zimesababisha mnara wa kusafrisisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 toka Singida, kupitia Namanga ukiwa umetitia ardhini hivyo kusababisha mnara huo kuvunjwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitoa.

Akizungumza baada ya kukagua eneo hilo, Mongela amewataka uongozi wa Kata ya Lengijave na wilayakusitisha shughuli zote za uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa TANESCO, wataalam wa miamba na wakandarasi wanao jenga mradi huo kuhakikisha wanakamilisha uchunguzi kasha kuharakisha ukamilishaji wa kazi ya ujenzi wa minara katika eneo hilo.

Mongela amesema, ‘‘haiwezekani kuendelea na shughuli za uchimbaji wakati kazi ya ujenzi wa minara hiyo ikiendelea kwani kufanya hivyo ni sawa na kuihujumu serikali ambayo imewekeza fedha nyingi katika mradi huu wa umeme wa msongo wa kilovolti 400’’

Mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongela na Kamati ya Ulinzi na Usalama wakiangalia eneo ambalo Mnara wa njia ya kusafirisha umeme ulititia ardhini kutokana na madhara ya uchimbaji mchanga katika Kata ya Lengijave na kusababisha mnara kuvunjwa ili kujengwa upya

Naye Meneja Usalama wa Mradi huo unao unganisha Tanzania na Kenya , Mhandisi Filbert Kajuna amesema sababu za mnara kutitia ardhini katika eneo hilo ni machimbo yamekuwa yakifanyika chini kwa chini jambo ambalo halikuwa rahisi kubaini uwepo wa matobo ya machimbo hayo. Baada ya kukamilika kwa ujenzi, mnara huo ulianza kutitia hivyo kulazimu mafundi kuanza kuuvunja ili kupata ufumbuzi wa tatizo la ardhi katika eneo hilo ili ujenga mnara mpya.

Baadhi ya wachimbaji wa mchanga pamoja na uongozi wa kata wamesema kufungwa kwa mgodi huo kutasababisha kukosekana ajira kwani vijana wengi wamejiajiri kupata kipato cha kuendesha maisha ya familia zao, lakini kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa pamoja na kuona athari zilizo jitokeza katika mnara huo hawana budi kusitisha uchimbaji hadi hapo serkali itakapo wapatia ufumbuzi wa tatizo hilo.