Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amewaasa wananchi wa mkoa huo ambao maeneo ya vijiji vyao yamepitiwa na mradi wa kusafirisha umeme unao unganisha nchi za Tanzania na Kenya, kuhifadhi na kulinda miundombinu ya umeme iliyo pita katika maeneo yao.
Mongela ameyasema hayo alipo tembelea eneo la machimbo ya mchanga yaliyopo katika Kata ya Lengijave, Wilaya ya Arumeru ili kujionea athari za uchimbaji mchanga ambazo zimesababisha mnara wa kusafrisisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 toka Singida, kupitia Namanga ukiwa umetitia ardhini hivyo kusababisha mnara huo kuvunjwa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitoa.
Akizungumza baada ya kukagua eneo hilo, Mongela amewataka uongozi wa Kata ya Lengijave na wilayakusitisha shughuli zote za uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo.
Mkuu huyo wa Mkoa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa TANESCO, wataalam wa miamba na wakandarasi wanao jenga mradi huo kuhakikisha wanakamilisha uchunguzi kasha kuharakisha ukamilishaji wa kazi ya ujenzi wa minara katika eneo hilo.
Mongela amesema, ‘‘haiwezekani kuendelea na shughuli za uchimbaji wakati kazi ya ujenzi wa minara hiyo ikiendelea kwani kufanya hivyo ni sawa na kuihujumu serikali ambayo imewekeza fedha nyingi katika mradi huu wa umeme wa msongo wa kilovolti 400’’
Naye Meneja Usalama wa Mradi huo unao unganisha Tanzania na Kenya , Mhandisi Filbert Kajuna amesema sababu za mnara kutitia ardhini katika eneo hilo ni machimbo yamekuwa yakifanyika chini kwa chini jambo ambalo halikuwa rahisi kubaini uwepo wa matobo ya machimbo hayo. Baada ya kukamilika kwa ujenzi, mnara huo ulianza kutitia hivyo kulazimu mafundi kuanza kuuvunja ili kupata ufumbuzi wa tatizo la ardhi katika eneo hilo ili ujenga mnara mpya.
Baadhi ya wachimbaji wa mchanga pamoja na uongozi wa kata wamesema kufungwa kwa mgodi huo kutasababisha kukosekana ajira kwani vijana wengi wamejiajiri kupata kipato cha kuendesha maisha ya familia zao, lakini kutokana na agizo la Mkuu wa Mkoa pamoja na kuona athari zilizo jitokeza katika mnara huo hawana budi kusitisha uchimbaji hadi hapo serkali itakapo wapatia ufumbuzi wa tatizo hilo.
More Stories
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania
Rais Samia apeleka Bil. 6 kuboresha sekta ya elimu Kaliua
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM