Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha
MKURUGENZI mpya wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), Christine Mwakatobe, ameanza kazi kwa kishindo baada ya maofisa waandamizi sita, wakiwemo vigogo watatu kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Mwakatobe aliteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa AICC, akichukua nafasi ya Ephraim Mafuru, ambaye Machi 15, 2024, aliteuliwa na Rais kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano AICC, Freddy Maro, ilielezwa kuwa wakurugenzi hao na maofisa hao waandamizi walisimamishwa kazi kuanzia Aprili 3, 2024.
Wachambuzi wa mambo yanaelezwa kuwa uamuzi huo uliochukuliwa na AICC, unatafsiriwa kuwa, Mwakatobe ameelewa ipasafavyo falsafa ya Rais Samia, ya kuwataka watendaji wakuu wa mashirika ya umma kutimize wajibu wao na kufanya kazi kwa weledi ili kuleta tija kwa Taifa.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo mwaka jana, Agosti 19 wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi na mashirika ya umma, mkutano ambao uliwajumuisha pia wajumbe wa bodi, mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine.
Wakati akitoa maelekezo hayo, Mwakatobe, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO) ambayo aliiongoza kuanzia Septemba 1, 2022.
Rais Samia alisema watendaji wa mashirika hayo, wanatakiwa kubadilika kifikra na hivyo kufanya kazi kwa weledi na hatimaye kuongeza mapato na tija kwa Taifa, badala ya mashirika hayo kuendelea kuwa tegemezi kwa Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Savo Mung’ong’o, Mkurugenzi wa Miliki na Miradi, Victor Kamagenge na Mkurugenzi wa Mikutano na Masoko, Mkunde Mushi.
Wengine ni Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu, Festo Mramba, Mhasibu Mkuu, Augustine Karadoga na Meneja wa Ukmbi wa Mikutan wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Catherine Ilinda.
Wakurugenzi watatu na maofisa wengine waandamizi amesimamishwa kwa muda ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kukiuka kanuni za uendeshaji wa mashirika ya umma.
“Taratibu zingine kuhusu uchunguzi huu zitatolewa hapo baadaye kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma,” imesema taarifa hiyo.”Ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, taarifa hiyo imesema huo ni utaratibu wa kawaida wa mashirika ya umma.
Akizungumza mara baada ya kushika wadhifa huo, Mwakatobe, alitaja mambo matano anayotarajia kuegemea katika uongozi wake ili kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya utalii wa mikutano.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kuongeza mapato ya taasisi hiyo, kubuni miradi mikubwa ya maendeleo, lakini pia kuboresha maslahi ya wafanyakazi wake na kuboresha huduma za taasisi hiyo za mikutano, hospitali na malazi.
Mwakatobe alisema anatarajia kuongeza vyanzo vipya vya mapato na kubuni miradi pia kuboresha zilizopo ikiwemo huduma ya mikutano, nyumba za malazi na Hospitali.
“Kujenga uhusiano mzuri baina ya wadau wa utalii na kuboresha huduma zetu, ni sehemu pia ya malengo yangu bila kusahau maslahi ya wafanyakazi wetu, kwani hayo ndio yatakayoleta uhalisia wa kitovu cha diplomasia ya mikutano na utalii pia” alisema Mwakatobe.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu