Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Morogoro
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amemuhakikishia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, kuwa katika Mpango na Bajeti ya Mfuko ya mwaka ujao (2021/2022), wamejikita zaidi katika vipaumbele saba.
Kwa mujibu wa Mshomba vipaumbele hivyo saba vinaenda kuondoa kero mbalimbali hasa za wanachama.
Mshomba ameyasema hayo mwishoni mwa wiki, wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la 47 la Wafanyakazi wa NSSF lililofanyika mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Mshomba, vipaumbele hivyo ni kama ifuatavyo;
Kuandikisha wanachama
Ametaja kipaumbele cha kwanza, ni kuhakikisha wanaandikisha wanachama katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi
Kuboresha huduma
Kipaumbele cha pili, Mshomba amesema ni uboreshaji wa huduma, kwani kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanachama, hivyo wameelekeza nguvu katika kulitekeleza hilo.
“Tutahakikisha mifumo yetu (NSSF), iko vizuri na inakidhi matarajio yetu, katika hili tutatumia Tehama kuhahikikisha kazi zetu zinakwenda vizuri na huduma kwa wateja zinatolewa,” amesema.
Mafunzo kwa wafanyakazi
Mshomba amesema kipaumbele cha tatu, ni mafunzo kwa wafanyakazi ili waweze kuelewa taratibu za Mfuko.
Mafunzo ya watoa huduma kwa wanachama
Kipaumbele cha nne, amesema ni mafunzo kwa wafanyakazi watoa huduma kwa wanachama ili waweze kuvaa viatu vya wanachama kwa kuzingatia maadili ya Mfuko.Kujenga timu moja
Amesema kwamba kipaumbele cha tano, ni kujenga timu mmoja kwani bila ya kuwa na timu moja katika Mfuko mkubwa kama huo wanaweza wasifikie malengo, hivyo watawafanya wafanyakazi kuwa sehemu ya mfuko huo.
Kuwekeza mazingira bora ya kazi
Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kipaumbele cha sita, wataweka mazingira bora ya kazi kwani ni jambo muhimu na kwamba amemuomba Waziri Mhagama kuwaunga mkono.
Usimamizi madhubuti wa menejimenti na Bodi
Kipaumbele cha saba, amesema ni usimamizi madhubuti hasa kwa Menejimenti na Bodi kwamba katika kutoa huduma bora lazima usimamizi uwe madhubuti ili waweze kufanikiwa katika malengo yao.
Kauli ya Waziri Mhagama
Akizindua Baraza hilo jipya la 47 la wafanyakazi wa NSSF, Waziri Mhagama, ameiiagiza Menejinti ya NSSF kuweka mifumo sahihi itakayoondoa changamoto za wanachama na wadau.
“Nawaomba mkatathimini mifumo iliyopo na ikiwezekana mtengeneze mifumo ambayo itamuwezesha mwanachama kulipwa mafao yake bila kwenda kupiga magoti kwa wafanyakazi wa NSSF,” alisema.
Waziri huyo amewataka watumishi kuendeleza kasi ya kukusanya michango ya wanachama kwenye maeneo yote ya ajira ili inapotokea mfanyakazi amepata janga lolote, Mfuko uweze kumlipa kwa wakati na bila ya usumbufu.
Kauli ya TUICO
Naye, Mwakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Viwandani, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) na Mkuu wa Sekta za Taasisi za Fedha, Willy Kibona, amesema maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mhagama yamekuwa ni funzo kwa Baraza hilo jipya pamoja na watumishi wote wa Mfuko na kuahidi kuyatekeleza na kuyazingatia kama alivyoelekeza.
Ameishukuru Menejimenti na wafanyakazi wote kwa ushirikiano walionao kwamba wanaendelea kuzingatia kanuni na taratibu za sheria ambazo Wizara inazisimamia.
“Tunasema asante sana wa kutujengea misingi imara ya kuanza tena awamu ya miaka mitatu ijayo ya Baraza hili hususani katika kutuasa yale yote ambayo tunatakiwa kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria ya NSSF,” amesema.
More Stories
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi
Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee
Watu 5,000 kuhudhuria tamasha la utamaduni Songea