Lubango Mleka, Timesmajira Online, Igunga.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imemkamata na kumfikisha katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Igunga aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Igunga Mjini (IGUWASA) Husseni Salumu Nyemba (34) akikabiliwa na tuhuma ya kesi Na. 1/2023 ya uhujumu uchumi.
Awali Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU kutoka Wilaya ya Nzega Mazengo Joseph akimsomea shitaka mshtakiwa Husseni Nyemba mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga Lydia Ilunda,ameiambia mahakama kuwa mshtakiwa Husseni Nyemba alitenda kosa hilo Julai, 2022.
Ambapo amesema mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji IGUWASA Wilaya ya Igunga kabla hajahamishiwa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Mazengo ameendelea kuiambia mahakama kuwa mshtakiwa Husseni Nyemba anakabiliwa na shitaka la uhujumu uchumi la kujipatia manufaa kwa njia zisizo halali kinyume na kifungu cha 23 (1) (a) na (2) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa cha 329 mapitio ya 2019 ikisomwa pamoja na sheria ya uhujumu uchumi.
Mazengo amesema kuwa  Julai, 2022 Mshitakiwa Husseni Nyemba akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji IGUWASA Wilaya ya Igunga alijipatia kiasi cha milioni nne toka kwa mfanyabiashara wa Jijini Dar es salaam, Rashidi Mwinyimkuu Mbegu ambaye alikuwa anadai malipo yake baada ya kutoa huduma ya vifaa katika mamlaka hiyo ya IGUWASA ambapo kiasi hicho cha milioni nne 4 kilitolewa ili aweze kulipwa fedha zake anazodai IGUWASA.
Hata hivyo baada ya kusomewa shitaka, mshtakiwa Husseni Nyemba alikana kutenda kosa hilo ambapo kesi hiyo imehairishwa hadi Mei, 16, 2023 kwa ajili ya hoja za awali baada ya upande wa Jamhuri kusema uchunguzi wa kesi hiyo umekamilika na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana ya milioni mbili 2.
More Stories
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa
Mgeja aipongeza CCM kwa uteuzi Wagombea Urais