May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuranga walalamikia zuio biashara ya mkaa

Na Mwandishi Wetu, Mkuranga

WAFANYABISHARA wilayani Mkuranga, wameiomba serikali kuruhusu biashara za uuzaji wa mkaa kwasababu wananchi wengi hawamudu gharama za kutumia gesi.

Ombi hilo limetolewa na mfanyabiashara Yasmin Kidawa, wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara (JWT) wilayani humo, mkoani Pwani, katika mwendelezo wa ziara ya kusikiliza kero za wafanyabishara.

Amesema kwasasa hawawezi kumudu gharama za kununua gesi, hivyo wakati wa kujipanga kuangalia namna ya kupunguza gharama za gesi wanaomba kuruhusiwa kwa matumizi ya mkaa.

“Tunafahamu nia ya serikali ni nzuri, lakini hali ya maisha ya wananchi wa huku Mkuranga ni ngumu, bado hatuwezi kumudu gharama za gesi. Tunaomba serikali ituache tuendelee kutumia mkaa badala ya kuzuia bila kuangalia hali yetu kiuchumi,” amesema Kidawa.

Naye mfanyabishara Jumanne Mohamed, amesema wananchi wa wilaya hiyo wanakabiliwa na changamoto kubwa ya umasikini.

Amesema biashara kubwa ya uchumi wilayani humo ni bidhaa za misitu lakini kutokana na kuzuiliwa kwa biashara ya mkaa, wamezidi kuwa masikini kwasababu wengi hawamudu bei ya mkaa lakini pia gharama ya gesi ni kubwa.

Amesema serikali inatakiwa kupunguza bei ya gesi ili kila Mtanzania amudu kutumia na kupunguza matumizi kuliko kuzuia matumizi ya mkaa kwa kuweka ushuru wa Sh. 6,000 kwa kiroba na gharama kubwa ya gesi.

Amesema gharama ya mkaa kwa kiroba kidogo ni Sh. 12,000 hadi 15,000 wakati awali wanununua kwa Sh. 3,000 hadi 4,000.

Aidha, wamewalalamikia maofisa wa Wakala wa Misitu (TFS), kuwanyang’anya wafanyabishara wa mkaa mizigo yao na kuiuza badala kuiteketeza.

“Kama mmepiga marufuku uuzaji wa mkaa, mnapowanyang’anya wafanyabishara iteketezwe sio wanaichukua na wao wanaenda kuiza maana yake ni kutumwamisha sisi lakini siyo kuzuia biashara ya mkaa,” amesisitiza .

Mwenyekiti wa JWT, Hamis Livembe, ameahidi kuifikisha kero hiyo ngazi ya halmashauri ili zifanyiwe kazi na wenye mamlaka.