Na Esther Macha, Timesmajira Online – Kyela
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya (Mbeya UWSA) kwa utekelezaji bora wa miradi ya maji, akisema juhudi hizo zimeendelea kujenga imani kwa wananchi kuhusu serikali yao.
Ussi ametoa pongezi hizo Oktoba 11, 2025, wakati akikagua mradi wa upanuzi wa huduma ya maji katika Kata ya Ipinda, wilayani Kyela, mkoani Mbeya.
“Ndugu zangu wa Ipinda, Mwenge wa Uhuru umejionea mwendelezo wa uboreshaji wa miundombinu ya maji katika eneo hili tumeona kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira pamoja na Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA),” amesema Ussi.
Ameongeza kuwa, katika Halmashauri zote 193 walizopita, wamejionea utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta ya maji, na kwamba hayo yote yanaonyesha dhamira ya dhati ya serikali ya kuwaletea wananchi huduma bora.
“Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, anayo kila sababu ya kujivunia mafanikio haya katika usambazaji wa maji mijini na vijijini. Tuliyoyaona hapa Ipinda yamezidi kujenga imani kwa wananchi,” amesema.
Ussi pia amewawasihi wananchi kushiriki kikamilifu kulinda miundombinu ya maji katika maeneo yao ili miradi hiyo iwe endelevu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase, amesema mradi huo ulianzishwa mwaka 1980, lakini kutokana na ongezeko la watu, serikali iliamua kuupanua ili kukidhi mahitaji ya sasa.
“Tayari zaidi ya kilomita 20,000 za mabomba yamelazwa, na zilizobaki kilomita saba zitaendelea baada ya vifaa kuwasili kupitia ufadhili wa Rais Dk. Samia,” amesema Manase.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kasulumu Kyela Mhandisi Raphael Kolong’onyo, amesema mradi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji kwa gharama ya Sh milioni 705 chini ya usimamizi wa Mbeya UWSA.
Amesema mradi huo unahusisha ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 27, ujenzi wa kituo cha kuchotea maji, ukarabati wa bomba kuu kutoka Ipinda hadi Tenende, pamoja na matanki mawili ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 50,000. Pia unahusisha ununuzi wa dira za maji 500 na vifaa vya kufuatilia ubora wa maji.
“Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 55, na tayari wananchi wameanza kunufaika na huduma hii muhimu,” amesema Kolong’onyo.

More Stories
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini
REA imeleta mageuzi sekta ya nishati