November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkenge ataka wadau kuendeleza michezo

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Muharami Mkenge amewataka wadau wa michezo jimboni hapa kuhahasisha wanaanzisha vyama mbalimbali kwa lengo la kuibua na kuendeleza vipaji husika.

Mkenge ameuambia Mtandao huu kuwa, katika maeneo mengi aliyopita amewashuhudia vijana kwa wazee wakishiriki michezo tofauti ikiwemo soka, netiboli, drafti, bao, karata na michezo kadhaa lakini imekuwa haina maendeleo kutokana na kukosekana kwa vyama.

Amesema, mfano mzuri ni kwenye upande wa soka mchezo ambao umekuwa na vipaji vingi vinavyokosa nafasi ya kuendelezwa hivyo ni vyema ukaandaliwa utaratibu wa kuwakutanisha wadau mbalimbali na kisha kuunda uongozi utakaokuwa na jukumu la kuusinamia na kuuendeleza mchezo huo.

“Kulikuwa na vyama vilivyokuwa vinasimamia mpira wa miguu kwa vijana kuanzia miaka 17 pale Temeke, Dar es Salaam ambacho kilikuwa kinaitwa (TEDIYOSA) Kinondoni (KIDIYOSA) na Ilala (IDIYOSA) vilivyokuwa vinaendeleza vipaji vya vijana na hapa Bagamoyo nataka BAGADIYOSA kiundwe, ” amesema Mkenge na kuongeza.

“Ni matumaini yangu kuwa wadau wa mchezo huu na mingine wana maeneo wanayokutana kwa ajili ya michezo yao, niwaombe waunde vyama vya michezo husika nami nitapanga tukutane ili tupange mikakati ya namna gani kwa pamoja tutavyoweza kushirikiana,”.

Pia mbunge huyo amezitakia timu zinazotokea kwenye jimbo hilo zinavyoshiriki Ligi soka ngazi ya Mkoa vipambane ili kufanya vizuri katika michuano hiyo ili kutwaa ubingwa huo kwa mwaka huu.

“Nina imani na viongozi wa timu zinazoshiriki, makocha, wachezaji, wadau pamoja na uongozi wa BFA ambao watashirikiana ili mwaka huu ubingwa wa Mkoa wa Pwani ubaki Bagamoyo, hii itakuwa faraja kubwa sana kwangu,” amesema Mkenge.

Katika Ligi hiyo timu tano kutoka jimbo la Bagamoyo ni Baga Friends, Baga United, Dunda United na Kiembeni zote zikitumia uwanja wa Mwanakalenge wakati Mwambao SC ikiwa katika uwanja wa Msoga jimbo la Chalinze.