May 14, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkakati ondoshaji ongezeko la shehena yatajwa

BUNGE  limepitisha bajeti ya shilingi trilioni 2.87 ya Wizara ya Uchukuzi  kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ambapo pamoja na mengine bajeti hii inakwenda kutekeleza miradi mbalimbali inayohudumiwa na wizara hiyo ikowemo kukabiliana na ongezeko la shehena bandari ya Dar Es Salaam.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma Waziri wa Uchukuzi Profesa Mbarawa Mnyaa Mnyaa amesema katika kipindi hicho  Wizara yake inakwenda kukabiliana na ongezeko la shehena hasa katika vandari ya Dar Es Salaam kwa  kuboresha miundombinu ya bandari, reli na maeneo ya kuhifadhi mizigo ili kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha biashara ya kikanda na kimataifa.

Aidha , Profesa  Mbarawa amesema,Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kuingia bandarini kupitia mradi wa Port Link pamoja na ujenzi wa eneo la kupakilia mizigo kwenye treni za SGR katika eneo la Malindi Marshalling Yard.

Amesema hatua hizo zinalenga kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

“Serikali pia imekamilisha ujenzi wa kituo cha mizigo Morogoro kitakachounganishwa na reli ya SGR katika eneo la Stesheni ya Morogoro,” amesema Profesa Mbarawa.

Amefafanua kuwa kituo hicho chenye ukubwa wa mita za mraba 68,000 kitakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 600 kwa siku na kitasaidia kusafirisha mizigo kwenda mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Ruvuma na Dodoma pamoja na nchi jirani za Zambia na Malawi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, uondoshaji wa mizigo kutoka eneo la Malindi kupitia reli ya SGR kwenda Kituo cha Mizigo Morogoro unatarajiwa kuanza mwezi Juni 2026.

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imeanza ujenzi wa magati mawili mapya katika eneo la Malindi, Bandari ya Dar es Salaam, yatakayokuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni tatu za ziada za shehena kwa mwaka.

Amesema magati hayo ni sehemu ya mpango wa kujenga magati 10 mapya ili kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mizigo inayoongezeka.

“Kati ya magati hayo, manne yataanzia gati namba 12 hadi 15 katika eneo la Kitopeni-Kurasini huku mengine sita yakijengwa Vijibweni-Kigamboni kuanzia gati namba 16 hadi 21,” amesema.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza idadi ya magati katika Bandari ya Dar es Salaam kutoka 12 yaliyopo sasa hadi kufikia 22.

Aidha, alisema Serikali inaendelea na upanuzi wa eneo la Kurasini Port Extension lenye ukubwa wa mita za mraba 220,000 kwa ajili ya kuhudumia makasha, ambapo eneo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia makasha 700,000 kwa mwaka.

Profesa Mbarawa amesema awamu ya kwanza ya mradi huo yenye uwezo wa kuhudumia makasha 150,000 imefikia asilimia 92 ya utekelezaji, huku awamu ya pili ikitarajiwa kuanza Juni 2026.