November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya maji ya Bil 10 yatekelezwa Buhigwe

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Buhigwe

SERIKALI imesikia kilio cha wakazi wa Wilaya ya Buhigwe, Mkoani Kigoma na kutoa zaidi ya sh bil 10 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika Vijiji na Kata ili kupunguza kero ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Meneja wa RUWASA Wilayani humo Mhandisi Golden Katoto alisema maeneo mengi ya wilaya hiyo yalikuwa hayajafikiwa na huduma ya maji safi na salama hali iliyopelekea wananchi kutumia maji ya mito na visima yasiyo salama.

Alisema kwa kulitambua hilo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 serikali ya awamu ya 6 imewapelekea fedha kiasi cha sh bil 10.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi 4 ya maji katika Vijiji na Kata zaidi ya 8 ili kupunguza kero hiyo.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni ule wa Kilelema unaogharimu sh bil 1.1 ambao utekelezaji wake sasa uko katika hatua za mwisho na unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 10,000 wanaoishi katika vijiji mbalimbali na kata zilizo jirani.

Mhandisi Katoto alitaja mradi mwingine kuwa ni wa Mnanila-Nyakimwe unaogharimu sh bil 8.3 ambao utahudumia wakazi wa vijiji mbalimbali ikiwemo Nyakimwe, Mnanila, Bweranka, Kibande na Kitambuka.

Alisema utekelezaji mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 50 na unahusisha uchimbaji wa visima na usambazaji maji kwa watumiaji, ambapo aliitaka jamii kutunza miundombinu ya miradi hiyo ili idumu na kuwanufaisha wananchi wengi .

Mradi mwingine ni wa Buhigwe-Kavomo-Mlera  unaogharimu kiasi cha sh bil 1.6 ambao utekelezaji wake upo katika hatua za mwishoni ukihusisha maboresho ya chanzo cha maji Nyafisi na ujenzi wa matenki katika vijiji husika.

Alibainisha kuwa takribani vijiji 29 kati ya 44 vina miradi ya maji safi na salama, 11 vinatumia maji ya visima vilivyoboreshwa na 4 bado havijashafikiwa na huduma hiyo.

Mhandisi Katoto alilieleza gazeti hili kuwa wamedhamiria kufikisha huduma ya maji safi kwa wakazi wa vijiji na kata zote zilizopo katika wilaya hiyo na kubainisha wazi kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutapanua wigo wa upatikanaji huduma ya maji safi kutoka asilimia 72 hadi 90.2.

Mkazi wa Kijiji cha Bweranka Yustas Nzogela alipongeza serikali ya awamu ya 6 kwa kupeleka mabilioni ya fedha katika wilaya hiyo mpya kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na kuongeza kuwa kero ya maji katika wilaya hiyo itabaki historia.

Wakazi wa Wilaya ya Buhigwe, Mkoani Kigoma wakifurahia mradi wa maji safi na salama uliotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika kijiji chao. Picha na Allan Vicent