Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Bukoba
MIGOGORO ya ardhi mkoani Kagera inadaiwa kuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani kwa wananchi pamoja na mauaji.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia jenerali Marco Gaguti katika tukio la kuwaapisha wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Bukoba mkoani humo.
Brigedia Jen.Gaguti ,amesema Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa yenye changamoto nyingi za migogoro ya ardhi.
Amesema kuna jumla ya mashtaka 896 ya migogoro ya ardhi mwaka huu kati ya mwezi Januari na Agosti mwaka huu kesi zilizofunguliwa ni 478,ambazo hazijaamuliwa 201 ,rufaa 159 hazijaamuliwa na mashauri 536 .
Amesema kutokana na idadi ya kesi hizo za ardhi mkoa upo katika hatari kushuka au kupotea kwa suala la ulinzi na usalama.
Amesema ipo changamoto ya usalama katika Mkoa wa Kagera na kudai kuwa mambo ambayo yamesababisha mauaji ni migogoro ya ardhi pamoja na mirathi.
Amesema katika mirathi pia ukienda kwenye chimbuko la mgogoro utakuta ardhi ina sehemu kubwa matokeo yake kumekuwa na uvunjifu mkubwa wa amani kutokana na wananchi kujichukuliwa sheria mkononi.
Awali Kaimu Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Fahamu Mtulya, amesema wajumbe hao wameapishwa ili waweze kumsaidia mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba, Mkoa wa Kagera.
Jaji Mtulya, amesema majukumu makubwa ya wajumbe ni kumsaidia mwenyekiti wa baraza hilo kufikia haki.
“Nyinyi mnapeleka vionjo vya wananchi kwenye uongozi wa mahakama,mwenyekiti anategemea mtazamo na uhalisi wa kilichotokea kwenye mgogoro na lazima achukue maoni ya wajumbe asipofanya hivyo uamauzi atakao utoa utakuwa batili”amesema jaji Mtulya.
Amesema haki ya ardhi ni haki ya msingi sana bila ardhi hakuna maendeleo ,hakuna nyumba wala chochote kitakacho tokea na kila kinachoongelewa katika maendeleo kinataokana na ardhi.
Hata hivyo amewasisitiza kutokujihusisha na vitendo vya rushwa hali ambayo inachangiwa kwa kiasi kikubwa uwepo wa malamaliko katika vyombo vya maamuzi.
Kwa upande wa wajumbe walioapishwa katika baraza hilo wamesema kuwa watazingatia sheria kanuni na miongozo ya baraza la ardhi na nyumba ili kutimiza wajibu wao.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani