Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe, amezindua Mfumo wa Huduma za Serikali (Government Service Directory – GSD) pamoja na Mfumo wa Kudhibiti Usalama wa Mifumo ya Serikali (NGAO).
Ambapo amesema mifumo hiyo inalenga kuimarisha upatikanaji na utoaji wa huduma za Serikali kwa njia za kidijiti, sambamba na kuimarisha usalama wa mifumo na taarifa za Serikali katika mazingira ya teknolojia yanayoendelea kukua.
Prof. Shemdoe amezindua mifumo hiyo jijini hapa juni 23, 2026 wakati akifunga Wiki ya Utumishi wa Umma kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka,ambapo ilianza Juni 16 na kuhitikishwa Juni 23,2026 katika viwanja vya Chinangali Park.
Ameeleza kuwa mfumo wa GSD utawawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali za Serikali kupitia dirisha moja kwa urahisi na kwa wakati, huku mfumo wa NGAO ukiimarisha usalama wa taarifa za Serikali kwa kutumia teknolojia ya uthibitishaji wa vipengele vingi (Multi-Factor Authentication) kwa watumiaji wa mifumo hiyo.
“Mfumo wa GSD umesanifiwa na kutengenezwa na Ofisi ya Rais – UTUMISHI kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), na mfumo wa NGAO umesanifiwa na kutengenezwa na e-GA,”amesema.
Pamoja na hayo Prof. Shemdoe ametoa wito kwa e-GA kuendelea kusimamia uunganishaji wa mifumo ya Serikali ili kuhakikisha taasisi za umma zinabadilishana taarifa kwa ufanisi, kupunguza urudufu wa taarifa na kuongeza tija katika utoaji wa huduma.


More Stories
Wananchi watahadharishwa dhidi ya bidhaa bandia
RAS apongeza mfumo kudhibiti upotevu wa mafuta
Kampuni za Algeria zasaka wabia wa biashara nchini