May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Samia yang’arishaTanzania kwa mtandao bora wa barabara Afrika


Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline Mwanza

UONGOZI wa miaka mitatu wa Rais Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye mtandao bora wa barabara, ambazo kwa sehemu kubwa zinapitika majira yote.

“Hata pale mawasiliano ya barabara yanapokuwa yamekatika kutokana na mafuriko, Serikali imekuwa ikitoa fedha mara moja ili kurudisha mawasiliano kwa wakati na hivyo kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.”

Hayo yamesemwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati akieleza kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Samia.

Amesema kwa kutambua thamani na umuhimu wa barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Samia, imekuwa ikiimarisha uwezo wa kifedha wa kitaasisi ili kuzilinda barabara kwa lengo la kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.

Ameongeza kwamba Rais Samia amekuwa akitenga wastani wa sh. bilioni 850 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara hapa nchini.

Fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa wastani wa miradi 620 ya matengenezo ya barabara kwa barabara za Kitaifa na miradi 850 kwa barabara za wilaya kila mwaka.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikiimarisha uwezo wa taasisi zinazosimamia kazi za barabara, hususan TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara, kwa kuziongezea vitendea kazi pamoja na wataalam.

Amefafanua kwamba kuimarika kwa uwezo wa kifedha na kitaasisi kumewezesha matengenezo ya barabara kufanyika mara kwa mara, Kutokana na kufanyika kwa matengenezo hayo, zaidi ya asilimia 90 ya mtandao wa barabara za Kitaifa uko kwenye hali nzuri na wastani.

Aidha, amesema zaidi ya asilimia 60 ya mtandao wa barabara za Wilaya uko kwenye hali nzuri na wastani. Hivyo sehemu kubwa ya mtandao wa barabara unapitika kipindi chote cha mwaka.

Ametolea mfano kazi za dharura zilizofanyika maeneo ya Hanang (Manyara), Liwale (Lindi) na Ununio (Dar es Salaam).

“Kwa kuboresha miundombinu ya barabara, wananchi wamewezeshwa kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kama vile elimu, afya, masoko, ajira na fursa nyingine za kujipatia kipato,” amesema na kuongeza;

“Heko kwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt Samia kwa kuweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya barabara na hivyo kuiwezesha kutoa mchango unaotarajiwa kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi.”

Amesema mtandao wa barabara hapa nchini una jumla ya kilometa 181,602.2 zikijumisha kilometa 37,225.7 za barabara za Kitaifa na kilometa 144,376.5 za barabara za Wilaya.

Barabara za Kitaifa zinasimamiwa na TANROADS na barabara za Wilaya zinasimamiwa na TARURA.

Kutokana na hali ya jiografia ya nchi yetu, usafiri wa barabara ndiyo njia inayotumiwa zaidi kwa usafiri na usafirishaji. Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 90 na 80 ya abiria na mizigo, mtawalia, hutumia barabara.