August 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhitimu asiyeona aeleza mafanikio ya useremala VETA

Mhitimu asiyeona aeleza mafanikio ya useremala VETA

Na Joyce Kasiki, Tanga

MHITIMU wa Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Tanga, Ernest Igobeko, mwenye ulemavu wa macho (asiyeona), ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kuwajali watu wenye mahitaji maalum na kuendelea kuwa kinara katika kuwawezesha kupata ujuzi unaowapa ujasiri wa kujitegemea, kujiajiri na kuajiriwa.

Aidha Igobeko ameiomba Serikali imuwezeshe kuendelea na masomo katika ngazi inayofuata ili kuongeza zaidi ujuzi na maarifa aliyoyapata, akieleza kuwa hatua hiyo itamuwezesha kukuza uwezo wake katika fani ya useremala na kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kujitegemea.

Igobeko amesema mafunzo ya muda mfupi ya useremala aliyoyapata chuoni hapo yamemjengea uwezo wa kujitegemea na kumthibitishia kuwa ulemavu si kikwazo cha kujifunza na kufanya kazi za ufundi hivyo anahitaji kuendelea zaidi kukuza ujuzi wake.

Akizungumza leo, Agosti 23, mwaka huu, mbele ya Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, aliyetembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, yaliyofanyika katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, Igobeko amesema mafunzo hayo yamemjengea kujiamini na kubadili mtazamo wa jamii kuhusu uwezo wa watu wasioona.

Amesema kabla ya kupata mafunzo hayo, baadhi ya watu walikuwa na mtazamo kwamba mtu asiyeona hawezi kufanya kazi za useremala, lakini mafunzo aliyopata yamemwezesha kujifunza na kutengeneza bidhaa mbalimbali za useremala kwa kutumia mbinu zinazomsaidia kufanya kazi kwa ufanisi.

Amesema mafanikio hayo yameongeza kujiamini kwake na kubadili mtazamo wa familia yake pamoja na jamii kwa ujumla kuhusu uwezo wa watu wasioona katika kujifunza na kufanya kazi za mikono.

Amesema anaamini kuendelea na masomo kutampa nafasi ya kujifunza zaidi, kutumia mashine mbalimbali na kuongeza uwezo wa kuzalisha bidhaa, hatua ambayo itamuwezesha pia kuwasaidia vijana wengine wenye mahitaji maalum, hususan watu wasioona, kuamini uwezo wao na kutumia fursa zinazotolewa kupitia mafunzo ya ufundi stadi.

Kwa upande wake, CPA Kasore amewahakikishia watu wenye mahitaji maalum kuwa Serikali  itaendelea kuwawezesha kupata mafunzo ya muda mrefu ya ufundi, ikiwamo kugharamia ada, ili waweze kujenga ujuzi, kutumia vipaji vyao na kujitegemea.

Akizungumza na mmoja wa watu wenye mahitaji maalum aliyekuwa akijifunza ujuzi wa kutengeneza vifaa, Mkurugenzi wa Mafunzo amesema fursa za mafunzo zipo na wanaohitaji wanapaswa kujiandaa kuanza masomo kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia watu wenye mahitaji maalum nafasi za mafunzo na kugharamia ada zao, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wanapata elimu na ujuzi unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

“Jipange, Januari uanze masomo pamoja na mwalimu wako. Serikali itafanya utaratibu wa kukupatia ada kama ilivyo kwa wale walioanza mwaka huu,” amesema.

Amesema mafunzo hayo hayalengi kumwezesha mwanafunzi kutengeneza vifaa pekee, bali pia kumjengea uwezo wa kutumia mashine mbalimbali na kupata utaalamu wa kutengeneza vifaa vinavyoweza kuwasaidia watu wengine wenye mahitaji maalum.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, baada ya kukamilisha mafunzo, mhusika anaweza pia kupata fursa ya kuwa msaidizi wa mafunzo na kutumia ujuzi alioupata kuwafundisha watu wengine.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata fursa sawa za elimu, mafunzo na ajira, huku akiwataka wanufaika kutumia nafasi hizo kwa bidii.

“Usikate tamaa, kila kitu kinawezekana. Jipange kwa ajili ya mafunzo ili uweze kujifunza vitu vingi zaidi, kujua mashine mbalimbali na hatimaye uweze kuwasaidia wengine,” amesema.