May 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mhandisi Mahundi awahimiza wanawake kumuunga mkono Dkt.Tulia

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewahimiza wanawake kumuunga mkono Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini,Dkt. Tulia Ackson kwani ni kioo na darasa la uongozi kwa Tanzania .

Mhandisi Mahundi, amesema pia wana Mbeya wanajivunia Mbunge huyo ambaye ni mfano wa kuigwa katika uongozi na amekuwa alifanya jitihada na ubunifu wa kuwatumikia wananchi .

Mhandisi Mahundi amesema hayo Mei 10,2025 wakati aliposhiriki kukimbia mbio za kilomita 5, katika mashindano ya riadha Mbeya Betika Tulia Marathoni,zilizohitimishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt.Dotto Biteko katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Pia amesema,ameshiriki mashindano ili kuunga mkono jitihada za Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya,Ambapo Mbunge huyo ameenda mbali zaidi kwa kuwawezesha wananchi wengi bima ya afya.

Mtoto Sophia Sanga,amesema kila mwaka amekuwa akishiriki mashindano hayo ambayo yamemjenga kimasomo na kumpanua kiakili ikiwa ni pamoja na kujifunza vitu mbalimbali kupitia kwa watoto wengine na jinsi viongozi wanavyoshiriki michezo.