December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa.

CCM: Rais amewafaraji wafanyabiashara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini, Joseph Mgongolwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kuonyesha imani kubwa kwa wafanyabiashara mbalimbali nchini.

Pongezi hizo amezitoa mjini Iringa wakati akielezea juu ya namna ambavyo maagizo ya Rais Samia kwa mamlaka husika yalivyoanza kuleta faraja na kuwapa nguvu wafanyabiashara kuendelea kufanya biashara zao nchini.

Amesema, Rais Samia ameonyesha njia nzuri kwani hata katika mazungumzo ya jana na mwekezaji Alhaji Aliko Dangote ambaye amewekeza katika kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa saruji mkoani Mtwara alimhakikishia kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wake na wawekezaji wengine unalindwa kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Hii ni hatua nzuri na muhimu sana kwa Taifa letu, tunaamini kuwa tukiwa na wawekezaji wengi ni fursa kubwa kwa ajili ya kujenga uchumi wetu na hata kufungua fursa nyingi za ajira kwa Watanzania. Tunaona namna ambavyo mwekezaji Dangote alivyowezesha kupitia uwekezaji wake hapa nchini kufungua fursa nyingi za kiuchumi, hivyo sisi wanachama wa CCM tutaendelea kumuunga mkono Rais Samia ili kuhakikisha Taifa letu linapata maendeleo kwa haraka,”amesema Mgongolwa.

Pia amesema, maagizo ya Rais Samia kwa mamlaka husika yamerejesha faraja kwa wafanyabiashara kwani kwa sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezifungulia akauti mbalim bali za wafanyabiashara ambazo zilikuwa zimefungiwa hapo awali, hivyo kwa hatua hii sasa wafanyabiashara watafanya kazi zao kwa bidii ili kujenga uchumi wao, Taifa na kufungua fursa za ajira zaidi,”amesema Mgongolwa.

Hata hivyo, Mgongolwa amewataka watumishi wa umma wakiwemo wa TRA kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi ili kuwezesha Taifa kusonga mbele, kwani baadhi ya watumishi kuendekeza urasimu tabia hiyo imekuwa ikizorotesha ukusanyaji wa mapato na hata wakati mwingie kuwasababishia maumivu wananchi na wafanyabiashara nchini.