April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgongano wa kikatiba wazuka Mahakama Kuu Zanzibar, Kesi za Wagombea Ubunge

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Mgongano wa kikatiba umejitokeza katika Mahakama Kuu ya Zanzibar kufuatia kesi zilizofunguliwa na waliokuwa wagombea wa Ubunge kupitia Chama cha ACT-WAZALENDO kwa majimbo 19 ya Unguja

Mgongano huo umeibuka leo mbele ya Jaji Hajji Suleiman Khamis katika Mahakama Kuu ya Zanzibar iliyopo Tunguu, wakati Mwanasheria mwanandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipodai kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar haina mamlaka ya kusikiliza mashauri ya wabunge yanayohusiana na mambo ya Uchaguzi.

Mwanasheria wa Serikali, Nalindwa Sekimanga, akiwa miongoni mwa jopo la wanasheria kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano, alitaja vifungu mbalimbali vya kisheria, ikiwemo Ibara ya 83 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kinachobainisha kuwa mashauri yote ya uchaguzi yanayohusu Wabunge yatasikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kutokana na hoja hiyo, Sekimanga aliomba Mahakama ikubali pingamizi lililowasilishwa na upande wa Serikali, akisisitiza kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar haina uwezo wa kikatiba kusikiliza mashauri yanayohusu mambo ya Uchaguzi wa Wabunge wa Jamuhuri.

Kwa upande wao, mawakili wasomi wanaowawakilisha waliokuwa wagombea Ubunge wa ACT-WAZALENDO, wakiongozwa na Wakili Msomi Omar Said Shaaban, alipinga hoja hiyo akieleza kuwa Mahakama Kuu ya Zanzibar ina mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusiana na Muungano.

Shaaban alikinukuu kifungu cha 93(1) cha Katiba ya Zanzibar na kifungu cha 3(1)(a) cha sheria Na.2 ya 1985 kuwa ndio kinachoianzisha, na kuipa mamlaka Mahakama Kuu ya Zanzibar na kwamba mamlaka iliyopewa ni bila ya Kikomo (unlimited) kwa mambo yote na sheria zote zinazotumika Zanzibar ikiwemo za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizotungwa na Bunge kama ilivyo sheria ya Uchaguzi. Hivyo Mamlaka ya Mahakama Kuu Zanzibar hayaondolewi wala hayapimiwi na Ibara ya 83 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika ngazi ya Mahakama Kuu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama imeahirisha kesi hizo hadi Januari 27, 2026, kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya pingamizi la kikatiba lililowasilishwa na wanasheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

k