January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgeja awapongeza machifu kumsimika Rais Samia kuwa chifu,awataka Watanzania kudumisha mila

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

WATANZANIA wameombwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha utamaduni wao ikiwemo kudumisha mila na desturi zenye maadili mema kwa mstakabali wa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Ombi hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa Tanzania Mzalendo Foundation yenye makazi yake mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na tukio la Rais Samia Suluhu Hassan kusimikwa uchifu mkuu wa watemi Tanzania.

Mgeja amesema nchi zote duniani zinazoheshimu, kudumisha, kuenzi, kurithisha utamaduni, mila na desturi zake zimepiga hatua kubwa kimaendeleo na kimaadili kwa kiwango kikubwa ambapo ametolea mfano mataifa ya China, Japan, Korea, India, Ujerumani na nyingine nyingi.

“Suala la kudumisha mila na desturi zenye maadili mazuri ni la muhimu kwa kila mtanzania, niwaombe sasa watanzania wenzangu tumuunge mkono Rais wetu, Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kudumisha tamaduni zetu,”

“Na nichukue fursa hii kuupongeza Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) kwa maamuzi yao ya busara yaliyotukuka ya kumsimika uchifu mkuu wa Machifu hapa nchini, Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, wamefanya jambo kubwa ambalo linaonesha jinsi gani wameamua kuuenzi utamaduni wetu,” ameeleza Mgeja.

Ameendelea kueleza kuwa heshima aliyotunukiwa Rais Samia ni adhimu kutokana na kuonesha gani umoja huo wa Machifu ulivyothamini mchango wake katika kuwaongoza na kuwatumikia watanzania chini ya Serikali yake ya awamu ya sita hali ambayo kwa upande wake itamuongezea nguvu ya kuwatumikia Watanzania.

“Na niseme wazi mimi binafsi nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye sasa amepewa jina rasmi la uchifu la Hangaya kwa kusimikwa kwenye nafasi hiyo ya uchifu mkuu, ni imani yangu ataendelea kutuongoza watanzania vizuri, na sisi ni jukumu letu kumuenzi kwa kudumisha tamaduni, mila na desturi zetu,” ameeleza.

Mgeja ambaye ni miongoni mwa wanafamilia wa wanangwa (wasaidizi) wa Chifu Kapela wa eneo la Kijiji cha Numbili, Tinde, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, amesema jina alilopewa Rais Samia la Hangaya (nyota njema) ni la kheri kubwa kwa Watanzania na lina falsafa pana ya kheri na mafanikio.

“Majina yote mawili yana kheri ya uongozi katika nchi yetu, maana ukiunganisha jina la Hangaya na Suluhu, moja linabeba heshima na mafanikio kama nchi na Watanzania wote, la pili linabeba suluhisho la changamoto zinazoikabili nchi na zinazogusa maisha ya Watanzania,” amefafanua Mgeja.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Shinyanga, na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), amesema majina mazuri ya viongozi yana manufaa kwa Taifa na hata dini zote huelekeza wazazi wawape watoto wao majina mazuri.

Mgeja katika kuonesha umuhimu wa Watanzania kuuenzi utamaduni wao amemnukuu pia Raia wa awamu ya kwanza, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye aliwahi kunukuliwa akisema, “Taifa lolote lisilokuwa na utamaduni wake, Taifa hilo huwa limekufa.”

“Hivi sasa Tanzania tulikuwa tukielekea huko na bahati nzuri tumempata rais msikivu na naamini hatutafika huko kwenye kuutelekeza utamaduni wetu na hatutokuwa Taifa mfu chini ya Chifu Hangaya, Rais Samia Hassan Suluhu,” ameeleza Mgeja na kuongeza;

“Kama nchi tukitaka kuwa na viongozi wazalendo na waadilifu ni muhimu wakatokana na malezi yanayozingatia mila, desturi na maadili yakiwemo ya dini na wala tusidanganyane, hatuwezi kupata viongozi waadilifu, wazalendo iwapo hawataandaliwa kwenye misingi ya malezi na makuzi mema mapema.”

Ameendelea kueleza kuwa ana imani kwamba Serikali ya awamu ya Sita chini ya Chifu Hangaya (Rais Samia) itafanyia kazi maombi yote yaliyotolewa na machifu wakati wakimsimika kuwa Chifu mkuu wa Machifu hapa nchini.

“Kwa hili la serikali kuonesha dhamiri ya kuwa karibu na machifu ni mwanzo mzuri, hatua hivyo inastahili pongezi na mengine yatafuata ikiwemo Taifa kudumisha ushirikiano na machifu wetu pamoja na kuwa utamaduni imara haya yanawezekana, hivyo twende pamoja kulijenga taifa letu.” amesema Mgeja.