Na Suleiman Abeid, TimesmajiraOnline,Shinyanga
TIMU ya Mpira wa Miguu ya JKT Tanzania imetangaza rasmi kuutumia uwanja wa CCM Kambarage kama uwanja wake wa nyumbani ambapo mechi yake ya kwanza itakuwa Ijumaa ya wiki hii kati yake na timu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mkoani Shinyanga, Ofisa habari na mawasiliano wa timu hiyo, Massau Bwire amesema wameuchagua uwanja huo wakiamini ni sehemu sahihi kutokana na wananchi wake kuwa na uzoefu wa kuhudhuria mechi za Ligi Kuu Tanzania.
Amesema mechi zote za nyumbani za JKT Tanzania zitachezwa katika uwanja huo wa Kambarage na hii inatokana na uwanja wao halisi wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni Jijini Dar es Salaam kuwa katika matengenezo makubwa kwa sasa.
Bwire amesema tayari Kamati ya TFF imeuthibitisha na kuupitisha uwanja huo wa CCM Kambarage na kuafiki kwamba umekidhi viwango vya kutumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Tanzania.
Amesema katika mchezo wao wa Ijumaa wiki hii wanatarajia kupata matokeo mazuri kutokana na wachezaji wake kujiandaa vyema ambapo amewatoa hofu wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na hofu yoyote kutokana na kupoteza michezo miwili ya awali.
Amefafanua kuwa chanzo cha kupoteza michezo hiyo miwili kati yao na timu ya Young African na KMC zote za Jijini Dar es Salaam kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na kukabiliwa pia na maandalizi ya mchezo mwingine mkubwa wa timu ya JKT Queen iliyokuwa katika mashindano ya CECAFA.
“Maandalizi ya timu ya JKT Tanzania ni mazuri, wachezaji wote wako vizuri tunakuja na mtindo mpya wa kichapo cha
“Double K” na huu utashughulika na kila atakayekuja mbele yetu lengo ni kuanza kupata matokeo chanya, tuna wachezaji bora na makini na wenye uwezo wa kupata matokeo mazuri,”
“Kila mmoja anayekuja kucheza hapa ajue hapa kuna Double K na hii itashughulika na kila tutakayekutana naye, na hatimaye tuanze kumvuta mmoja mmoja kati ya wale ambao wametutangulia na sisi tuelekee ambako tunakutarajia,” ameeleza Bwire.
Ametoa wito kwa wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga kuwaunga mkono wakati wote pale wanapokuwa na michezo kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa sasa na wasiwe na hofu yoyote ya matokeo ya michezo iliyopita kwa vile walikuwa wameshitukizwa lakini kwa sasa wamejipanga vizuri na wataonesha maajabu baada ya kushituka.
More Stories
15 wajinoa Juventus,akiwemo mtoto wa Mwenyekiti wa CCM Mbeya
Za Kwetu Fashion Show, yawapaisha wanamitindo nchini
TCAA yaadhimisha siku ya usafiri wa anga Duniani kwa kushiriki mbio za Marathon UDSM