December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mdau aweka wazii sababu ndoa za utotoni hususani katika mialo

Judith Ferdinand,TimesMajira Online

Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009,ina mueleza kuwa mtoto ni mtu yoyote mwenyewe umri chini ya miaka 18.

Pia inaeleza kuwa ulinzi wa mtoto ni kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya kikatili ambavyo vinaweza kuathiri mfumo wa ukuaji na maendeleo ya mtoto kiakili,kimwili na kisaikolojia.

Ambapo vitendo vya ukatili ni pamoja na ndoa za utotoni,mimba za utotoni ,kubakwa, kulawitiwa ,kupigwa, utumikishwaji katika umri mdogo,usafirishaji haramu wa binadamu na mengine.

Vilevile sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, inaeleza kuwa ulinzi wa mtoto unapaswa kuanza katika ukuaji wa mtoto kabla na baada ya kuzaliwa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 kila mtu anayo haki ya kufaidi haki za msingi za binadamu huku serikali itafanya jitihada kuhakikisha kwamba watu wote wanapata fursa sawa na za kutosha kuwawezesha kupata elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za shule na vyuo vingine vya mafunzo.

Mbali na sheria,sera na Katiba pia Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Haki za Mtoto (CRC),1989 na Mkataba wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa 1990 ni miongoni mwa jitihada za kuhakikisha mtoto anapata haki yake na kuondokana na vitendo vya ukatili ikiwemo ndoa za utotoni.

Mdau wa kutetea haki za wanawake na watoto anena sababu za ndoa za utotoni

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la Kivulini Yassin Ali, akizungumza na majira  na Times Majira Online kwa njia ya simu anaeleza kuwa, shirika hilo kwa sasa linafanya kazi katika mikoa ya Mwanza,Mara, Shinyanga,Geita na Kigoma.

Mkurugenzi wa shirika la Kivulini Yassin Ali, akizungumza katika moja ya warsha mkoani Mwanza.picha kwa msaada wa mtandao

Ambapo anaeleza kuwa   sababu ya kufanya kazi katika mikoa hiyo ni kwa mujibu wa takwimu ya Taasisi ya Takwimu ya Taifa kuwa  mikoa hiyo ndio inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Yassin anaeleza kuwa, takwimu za Taasisi  ya Utafiti  wa Idadi ya watu na Afya Tanzania (TDHS) ya mwaka 2015-2016,inaeleza kuwa kwa upande wa ndoa za utotoni mikoa inayoingoza ni Shinyanga kwa asilimia 59,Tabora asilimia 58,Mara asilimia 55 na Dodoma asilimia 51.

Anaeleza kuwa mimba za utotoni  zinamahusiano makubwa sana na ndoa za utotoni ambapo Mkoa wa Katavi unaongoza una asilimia 45,Tabora asilimia 43,Dodoma asilimia 39, Morogoro asilimia 39,Mara asilimia 37 na Mwanza asilimia 28.

Sabubu zinazochangia ndoa  na mimba za utotoni

Yassin anaeleza kuwa chimbuko linalochangia ukatili wa kijinsia,mimba na ndoa za utotoni ni hali ya chini aliyopewa mwanamke na mtoto wa kike kutokana na mila na desturi kandamizi.

Kutokana mila na  hali ya chini aliyopewa mwanamke na mtoto wa kike wanatumia kwa tamaa zao kutaka mtoto wa kike aolewe wapate mahali hususani kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo inaongoza kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vitendo vya ukatili mfano Shinyanga na Mara.

“Utaona inakiwango kikubwa cha mimba za utotoni na ndoa za utotoni,kwamba tamaa ya mahali ya wazazi au walezi,ni moja ya sababu inayochangia watoto wengi wa kike kuwa katika shinikizo la ndoa za utotoni,”anaeleza Yassin.

Anaeleza kuwa kwa  sababu ya sera na msukumo wa serikali ya kuhakikisha watoto wote wanaandikishwa shule,mfano katika mikoa ambayo shirika hilo linafanya kazi ikiwemo Shinyanga,Mara,Mwanza inafika mahala wazazi wanawatishia watoto wa kike siku za mitihani wafanye vibaya(wajifelishe).

“Kuna kauli ya kuwa nenda ukachore jovijo yani ni kuchora madudu aidha kwenye mtihani wa taifa wa darasa la saba,kidato cha pili au cha nne, kwaio kama  ulitoka kwenye kitovu cha tumbo langu uhakikishe haufaulu ole wako ujifanye una akili,”anaeleza Yassin kuwa hizo ndizo kauli wanazotumia baadhi ya wazazi kuwatisha watoto wao.

Yassin anaeleza kuwa wazazi wanajua  akishindwa (akishafeli) kwenye mtihani wa darasa la saba,kidato cha pili au cha nne itakuwa ni rahisi kutimiza adhima yao ya kupata mahali na kumuozesha binti.

Pia anaeleza kuwa umaskini ni sababu ya ndoa za utotoni kwani unakuta watoto wengi wa kike wanaotoka katika kaya maskini hawawezi kuendelezwa kielimu   kwa sababu familia  inakuwa na upendeleo kati ya mtoto wa kike na kiume katika suala la elimu.

Aidha anaeleza sababu nyingine ni watoto wengi kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi ambayo itawasaidia katika kujitambua,kujilinda dhidi ya mimba za utotoni au ndoa za utotoni.

Vilevile sababu nyingine ni jamii kunyamazia vitendo hivyo vya ukatili kwa sababu ndoa za utotoni ni moja ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Kwenye maeneo ya mialo watoto wa kike wapo kwenye hatari kubwa sana ya kuingia kwenye vishawishi  na kuangukia kwenye ndoa za utotoni kutokana na mazingira hayo na mifumo iliopo ya jamii kunyamazia na kuhalalisha vitendo vya ukatili,”.

Vilevile Yassin anaendelea kueleza kuwa sababu nyingine ya watoto wa kike kuingia kwenye ndoa za utotoni ni kutokana na wazazi kuwaogesha watoto wao wa kike dawa za kuwa na mvuto kwa wanaume.

Ambapo anaeleza kuwa mkoani Shinyanga kulikuwa na changamoto ya watoto wa kike kwenda kuogeshwa dawa maarufu kama samba kwa ajili ya kuvutia wanaume.

“Shinyanga ina kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni na shida iliopo ni baadhi  ya wanawake(mama) wenyewe wanatoa pesa kupeleka watoto wao wa kike kuogeshwa dawa hiyo ili kuvutia mwanaume,”anaeleza Yassin na kuongeza kwa kuhoji kuwa

“Mtoto anaendaje kuogeshwa hiyo dawa,tumeweza kutoa elimu ya madhara na kuweka mifumo,kanuni na taratibu ambazo zimepunguza tabia na mienendo ya kuchochea ndoa za utotoni,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Kivulini azungumzia maeneo ya uvuvi na changamoto ya ndoa za utotoni

Yassin anaeleza kuwa,katika maeneo ya uvuvi shinikizo kubwa ni kuwa na kiwango kikubwa cha wanaume(baba)  kutelekeza  familia kutokana na ukatili na umaskini kwa kushindwa kulea familia.

eneo moja wapo la shughuli za uvuvi zikiendelea picha kwa msaada wa mtandao

Hivyo jukumu la kulea familia wanaachiwa wanawake(mama) ambao uwatuma watoto wadogo wa kike kwenda kwenye mialo kufuata samaki akiwa na fedha ndogo.

Hali hiyo inachangia watoto wengi wa kike wakitumwa wanajikuta kwenye shinikizo la kukubali kufanya ngono isiyo salama ili apewe samaki na ile fedha ndogo aambiwe nenda kanunulie kitu kingine kwa sababu yeye ni rahisi na hana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.

Idadi kubwa wanayoishihudia maeneo ya mialo ni  utelekezwa wa familia ambapo hivi sasa wanawake nao wanatelekeza watoto na kuwaachia watoto wa kike wenye umri mdogo majukumu ya kuhakikisha mahitaji  ya nyumbani yanapatikana.

Hivyo na watoto hao katika kutimiza mahitaji ya kutafuta chakula wanajikuta wameingia kwenye mtego wa ndoa za utotoni na mimba za utotoni kutokana na vishawishi na shinikizo alilinalo la kutimiza mahitaji ya nyumbani.

“Utashangaa  tumefanya kazi kwenye baadhi ya Kata ambako kunafanyika shughuli za uvuvi ikiwemo Kayenze na Igombe,unaweza kukuta kwenye familia kuna binti mwenye umri wa miaka 18 hatumwi kwenda kununua samaki,bali atatumwa binti wa miaka 14 ambaye akienda yeye ndio hatakuja na samaki wengi hapo unapata picha gani? kwani ana akili zaidi ya dada yake mwenye umri wa miaka 18,” anahoji Yassin.

Harakati za shirika la Kivulini katika kuwaokoa watoto wa kike

Yassin anaeleza kuwa, shirika la Kivulini,wanajenga uwezo wa jamii na taasisi za kiserikali ili ziweze kuweka mifumo kuanzia ngazi ya kaya,kijiji,jamii,shuleni ambao utahakikisha unawalinda watoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni na ukatili wote.

Ambapo wametengeneza mfumo wa msaada wa elimu na sheria bure,ili kuhakikisha kwamba kama kuna mkakati wowote wa kumuozesha mtoto jamii inatoa taarifa kwa wakati iwe kwenye dawati la jinsia au kwa Mkuu wa Wilaya.

Mfumo huo umefanikiwa kunusuru watoto wengi akitolea  mfano Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza wameweza  kuwaokoa watoto wa kike zaidi ya kumi dhidi ya  ndoa za utotoni.

Yassin anaeleza kuwa watoto hao katika Wilaya ya Misungwi  mifumo ndio iliwezesha kuwakamata  wahusika  na kuwaokoa mabinti wakati wanaenda kutolewa mahali hivyo miongoni mwa visa hivyo  kisa kimoja ni cha mwanafunzi mmoja aliyekuwa kidato cha pili wazazi wakataka kumkatisha masomo ili aolewe.

Akisimulia kisa hicho Mkurugenzi huyo wa Kivulini Yassin, anaeleza kuwa binti huyo alipoona shinikizo limezidi sana la kutoka kwa baba na mama na tayari wameisha chukua mahali na kwamba wanamtishia kwamba akikataa watamlaani.

Aliwasiliana na wanaharakati na wasaidizi wa kisheria wa Kivulini wanaoenda nyumba kwa nyumba wanaishi huko ambao wapo 20 kila kata ambao walimueleza kuwa awaambie wazazi kuwa amekubali ila wakapime virusi vya Ukimwi na huyo mme mtarajiwa.

“Aliwaambia wazazi wake kuwa cha kwanza naomba twende kwenye vipimo,tumeisha fundisha kamati za ulinzi wa wanawake na watoto wamo watu wa afya,dawati,”.

Kwaio mtego uliowekwa wakati yule baba mwenye umri wa miaka 56 ameambiwa kuwa binti amekubali anataka mkapime afya alijua anaenda kupima afya kawaida na kurudi.

Lakini wakati wanaenda kule ndio aliweza kukamatwa na nyumbani ndio ulikuwa utoaji wa mahali kwaio binti aliweka kigezo kwamba warudishe mahali ila watakaporudi kutoka kwenye vipimo vya afya ndio wachukue mahali.

Na wakati wanatoa mahali kati ya wale waliokuwa wanashiriki katika zoezi la upokeaji mahali kulikuwa na wanaharakati wetu ambao walikuwa wanawasiliana vizuri na Polisi na Mkuu wa Wilaya.

“Tukio kama hili kwa mfano ni kuweza kuweka mifumo ndani ya jamii inayofichua na kutoa taarifa na kuweka mitego ni fundisho ambapo katika tukio hilo washiriki wanane waliweza kukamatwa na kufishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,”.

Yassin anaeleza kuwa  tukio lingine ni  la wanafunzi wengi ambao walikuwa katika maandalizi ya harusi hivyo kwenye kamati ya chakula kulikuwa na watu wao hivyo kufanya  sherehe hizo kuingiliwa na Polisi na ushahidi ukapatikana.

“Matokeo yanayotokea kwenye jamii kwa sababu  tumeweza kuwajengea uwezo wanaharakati ngazi ya jamii zaidi ya 2000 ambao wamekuwa wakitoa elimu dhidi ya ukatili,ndoa za utotoni na mimba za utotoni  na wamekuwa wakienda nyumba kwa nyumba, shuleni na nyumba za ibada na hii imesaidia kuimarisha mifumo,”.

Pia wameimarisha utendaji wa dawati la jinsia kupitia Kata kwa  kuweka ushirikiano na wanaharakati wa kujitolea na wasaidizi wa kisheria wapokuwa na jambo wanawaambia wanakuja haraka.

Aidha watoto wenyewe wamejitambua wanasema hapana dhidi ya ndoa za utotoni kuwa akiona tukio au viashiria vya ukatili atoe taarifa kwa mtu yoyote ambaye ataona  kuwa anaweza kumsaidia.

“Tulikuwa na kisa kimoja wazazi walivyoona binti anataka kukataa kuolewa  wakamfungia ndani ili asiwasumbue wakati waandaa kwa ajili ya kupika pilau kwa bahati nzuri viongozi wa serikali ya mtaa baada ya kupata  taarifa ile walishirikiana na sisi tulikwenda kumuokoa”.

Lengo ya haya yote ni  kuwajengea uwezo watoto wenyewe kuwa na  uelewa,kujitambua,kujilinda na kufichua vitendo vya ukatili kwani watoto wengi wanatishiwa na wazazi kuwa ukikataa kuolewa nitakulaani.

“Nimetolea mfano matukio hayo yaliofanyika kwa Wilaya ya Misungwi ambapo tumehakikisha mpaka sasa hivi wananchi wanaweza kuweka mitego na wakaita Polisi wakati wa zoezi la utoaji mahali au wakati wa harusi likiendelea baada ya  kugundua kuwa ni mtoto wa shule au mwenyewe umri chini ya miaka 18 kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na kuwakamata wahusika,”.

Ushirikiano wa Kivulini na Wizara ya Maendeleo Jamii,Jinsia na Watoto

Yassin anaeleza kuwa wanashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto kwa kutekeleza  mpango wa kitaifa wa kutokomeza ukatili huku moja ya shabaha ni kupunguza mimba za utotoni kutoka wastani wa asilimia 47 kitaifa mpaka asilimia 10 ambapo jambo hili wamelifanyia kazi kubwa sana katika mikoa ya Mara, Shinyanga,.

Yassin anaeleza kuwa,watu wamekuwa wakikwamisha jitihada za Serikali za kuwaletea watu maendeleo ya kielimu,ambapo inatoa fedha nyingi ya elimu bila malipo ambapo kwa sasa inatolewa kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha sita.

“Lakini ndoa za utotoni,mimba za utotoni ni kikwazo cha dhamira njema hii ya serikali,ya kuwawezesha watoto wa kike kufikia ndoto zao za kielimu na hatimaye waweze kunufaika na fursa za kiuchumi, kijamii,kimaendeleo,”.