May 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Busara za Serikali ya CCM zinahitajika kukinusuru Chama Kikuu cha Ushirika – SHIRECU.

Na Suleiman Abeid, TimesMajira Online

MOJA ya ahadi zilizomo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025 ni suala la kuimarisha vyama vikuu vya ushirika vilivyopo hapa nchini.

Inapozungumzwa neno ushirika inamaanisha kwamba, ni muungano wa watu ambao wanafanya kazi pamoja kwa hiari ili kufanikisha mahitaji yao ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kupitia shughuli inayomilikiwa kwa pamoja.

Vyama vya ushirika vimekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya Tanzania kwa zaidi ya miaka 75 iliyopita na katika kipindi hiki vimepata mafanikio mengi lakini pia changamoto nyingi na ni wazi katika kipindi hicho hakuna taasisi nyingine yoyote zaidi ya ushirika iliyowaunganisha pamoja watu wengi katika azma na lengo linalofanana.

Kumbukumbu zinaonesha baada ya Azimio la Arusha, vyama vya ushirika vilipewa kipaumbele katika kujenga moyo wa kujitegemea. 

 Hata hivyo kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa soko huria, vyama hivi vimekuwa vikijitahidi kushindana na sekta binafsi na vingi kushindwa kuwapa wanachama wake huduma wanazozihitaji.

Serikali kwa upande wake imekuwa ikilishughulikia tatizo hili ikiwemo kutunga Sera ya Maendeleo ya Ushirika (2002) ili kuvisaidia viweze kurudisha tena umuhimu wake katika maisha ya watu kiuchumi na kijamii.

Sera inaeleza jinsi serikali inavyopanga kuwezesha maendeleo ya eneo maalum la uchumi kama vile kilimo, elimu au ushirika ambapo sheria zinahitajika kuwezesha mipango hiyo kutekelezeka na zinaeleza jinsi ambavyo vyama vinavyopaswa kutenda katika njia ya kidemokrasia na ya kibiashara.

Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Ushirika, vyama vya ushirika ni vyombo huru na vinavyojitegemea chini ya uongozi na usimamizi wa wanachama wenyewe.

Tukirejea kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tunaona ikielezwa katika Ibara yake ya 33 juu ya umuhimu wa uwepo wa vyama vya ushirika hapa nchini kama ibara hiyo inavyoeleza, nanukuu;“Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaamini kuwa ushirika ni njia ya uhakika ya kuwezesha wanachama kuwa na uwezo mkubwa wa kutatua matatizo yote ya kiuchumi na kijamii kwa kutumia juhudi zao pamoja katika kufikia malengo ambayo yasingefikiwa kwa juhudi za mtu mmoja mmoja,” mwisho wa kunukuu.

Kutokana na ahadi hiyo, ilani hiyo katika Ibara yake ya 34 inaendelea kueleza kuwa, nanukuu;“….Katika kipindi cha miaka mitano (2020 – 2025) Chama Cha Mapinduzi kitahakikisha dhana ya ushirika wa hiari inajengwa na kusimamiwa na sheria ili kuwalinda na kuwanufaisha wanaushirika, hivyo kuchangia ipasavyo katika ustawi wao wa Taifa kwa ujumla.”

Na miongoni mwa kufikia mikakati hiyo, Ilani hiyo inaeleza kuwa ndani ya kipindi hicho cha miaka mitano, CCM itahakikisha vyama vikuu vya ushirika vinatekeleza majukumu yake na kuvihudumia vyama wanachama wake (Amcos) kwa kusimamia uzalishaji, upatikanaji wa pembejeo.

Huduma za ugani, masoko na kuajiri watendaji wenye sifa kwa kuzingatia ukubwa wa chama na miamala inayofanywa ili kuongeza ufanisi na usimamizi katika Vyama vya Ushirika.

Kuhakikisha vyama vya ushirika vinakuwa na uwezo wa kusimamia mifumo rasmi ya masoko ikiwemo stakabadhi za ghala kwa mazao yote hususani ya kimkakati na kuhamasisha mazao mengi kuingia kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala.

Kufufua na kuhamasisha vyama vya ushirika kumiliki viwanda ili kuongeza mnyororo wa thamani wa bidhaa zao kwa kufufua viwanda 262 ambavyo havifanyi kazi na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vipya 33 kwa mfumo wa makampuni yatakayomilikiwa na vyama vya ushirika na kuendeshwa kibiashara kwa maslahi ya wana ushirika.

Mpaka hapa tunaweza kuona jinsi gani Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya ilani yake hiyo ya uchaguzi kilivyoahidi kufanya juhudi kuhakikisha Vyama vya Ushirika hapa nchini vinafufuka na kuimarika kwa lengo la kuboresha maslahi ya wanachama wake.

Jengo la Makao Makuu ya SHIRECU mkoani Shinyanga.

Ni wazi kwamba itakuwa ni jambo la kushangaza ama kusikitikisha kukiona tena chama hiki (CCM) au baadhi ya wanachama wake wakipanda majukwaani na kuhubiri ama kuhamasisha habari za kuvunja au kuusambaratisha ushirika uliopo badala ya kuuimarisha kama inavyoelezwa ndani ya Ilani yake ya uchaguzi.

Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika vikongwe hapa nchini na katika miaka kadhaa kimekumbana na dhoruba za hapa na pale ikiwemo baadhi ya mali zake za kudumu kuuzwa “kinyemela” na viongozi wake waliopita waliokosa uadilifu.

Hata hivyo juhudi za Serikali ya CCM katika kuhakikisha SHIRECU inafufuka na kuimarika ziliwezesha mali nyingi zilizokuwa zimeuzwa “kinyemela” kurejeshwa mikononi mwa wana ushirika na kufufua matumaini ya ushirika huo kuanza kusimama imara baada ya kuchaguliwa kwa Bodi mpya ya Ushirika.

Katika awamu yake ya tano chini ya Hayati Rais John Magufuli, Serikali ya CCM iliweza kurejesha mali nyingi za vyama vikuu vya ushirika hapa nchini ambapo mbali ya SHIRECU pia iliweza kurejesha mali za Chama Kikuu cha Ushirika cha Mwanza (NCU), Chama Kikuu cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU), Kagera (KCU) na zile za Mamlaka ya Mkonge.

SHIRECU pamoja na kuwa miongoni mwa vyama vya ushirika vikongwe hapa nchini imekuwa ikikubwa na dhoruba kubwa za mara kwa mara za kumeguka vipande vipande hali inayoweza kusababisha kufanana na uliokuwa Muungano wa Kisoviet wa Urusi (USSR)  chini ya kiongozi wake Mikhail Gorbachev jinsi ulivyosambaratishwa.

Kusambaratika kwa uliokuwa muungano wa Kisoviet kulisababisha Mikhail Gorbachev kujikuta hana nchi ya kuongoza na hivyo kujing’atua mwenyewe madarakani, hali ambayo inaweza kutokea pia kwa SHIRECU iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka za kudhibiti njama zinazoendelea hivi sasa.

Hii inatokana na jinsi ambavyo wanachama wake wanavyojitenga na kuanzisha vyama vyao vipya vya Ushirika ikionesha wazi huenda ni “kansa” inayokitafuna chama hiki kidogo kidogo na hivyo Serikali ya CCM iliyoahidi kuulinda ushirika hapa nchini inapaswa kuitibu “kansa” hiyo kabla SHIRECU haijasambaratika kabisa.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa SHIRECU wakiwa kwenye mkutano wao mkuu wa mwaka.

Huko nyuma SHIRECU ilimeguka baada ya baadhi ya wanachama wake hasa wale wanaojihusisha na kilimo cha zao la tumbaku kule wilayani Kahama mkoani Shinyanga kuomba kujitenga na wakaweza kuanzisha Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU).

Lakini pia kuundwa kwa mikoa mipya ya Geita na Simiyu kulisababisha SHIRECU kuendelea kumeguka baada ya Wilaya za Bukombe na Bariadi kujitoa SHIRECU na kuanzisha vyama vyao ambavyo ni Chama Kikuu cha Ushirika cha Mbogwe na Bukombe (MBCU) na SIMCU kwa Mkoa wa Simiyu.

Ni wazi kujitenga na SHIRECU kwa waliokuwa wanachama wake kuliathiri kwa kiasi kikubwa uendeshaji wake na hivyo kujikuta kikihitaji nguvu ya ziada kuweza kujiendesha huku kikiwa kinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni na kushindwa kujiendesha kwa faida.

Katika hali ambayo inaonesha kuwashangaza waumini wa ushirika mkoani Shinyanga, ni kuona hivi sasa jinsi kundi lingine la wanachama wa SHIRECU linalotaka kujitenga na kuanzisha chama kingine kipya cha Ushirika cha Wilaya ya Kishapu.

Kundi hili linasemekana kuundwa na baadhi ya vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vipatavyo 46 kutoka wilayani Kishapu na tayari vimeanza harakati za kutaka kuandikishwa kwa Chama chao Kikuu cha Ushirika cha Ushirika wa Kishapu.

Maamuzi ya Amcos hizo 46 yanakuja wakati tayari SHIRECU inaonesha dalili za wazi za kufufuka na kuanza kujiendesha kwa faida tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma hali ambayo inawashangaza waumini sahihi wa ushirika mkoani Shinyanga wakihisi uamuzi huo unachangiwa na baadhi ya vigogo wilayani humo.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika (SHIRECU) mkoani Shinyanga, Kwiyolecha Nkilijiwa.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wanasema suala la kujitenga kwa Amcos za wilaya ya Kishapu lina dalili kubwa za ukanda wakifafanua kuwa vipindi vyote ambavyo SHIRECU iliongozwa na viongozi wakuu kutoka katika Wilaya hiyo huku ikiwa na hali mbaya zaidi hoja hiyo haikuwahi kuibuliwa.

“Binafsi mimi naamini hoja hii ya Amcos za Kishapu kujitenga ina harufu ya “Ukanda” maana kwa sasa viongozi walioko ndani ya SHIRECU wanatoka Wilaya ya Shinyanga, hawa wameonesha jinsi gani wameanza kuufufua ushirika wetu huu, zaidi ya miaka saba tukiwa chini ya viongozi kutoka Kishapu, hali yetu ilikuwa taabani,”“Chini ya viongozi hao, SHIRECU ilifikia kushindwa hata kuitisha mikutano mikuu ya wanachama, badala yake walikasimu kazi hiyo kwa Bodi, leo tunaanza kufufuka ndiyo inaibuliwa hoja ya kujitenga na kuwa na Chama Kikuu kingine cha Ushirika, Shinyanga tutakuwa na vyama vikuu vingapi jamani,” anahoji mmoja wa wana ushirika.

Mwanachama huyo wa moja za Amcos zilizopo Kishapu anashauri iwapo hoja za kujitenga inatokana na suala la kuwepo kwa bodi mbovu, ni vyema watu wakaweka wazi na wana haki za kisheria za kuitisha mkutano mkuu maalumu na kuwaondoa madarakani viongozi waliopo badala ya kugawanyika kwa kuunda chama kipya.

Inasemekana baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu na baadhi ya madiwani ambao pia wanatokana na CCM ndiyo wanaosimama kidete kutaka kuundwa kwa Chama Kikuu kipya cha Ushirika wa Kishapu na tayari imeundwa timu ya kwenda Dodoma kukutana na waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kushinikiza aridhie ombi lao.