April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jeneza lenye mwili wa Askofu na mbunge wa Viti maalum CCM Mkoa wa Morogoro mama Getrude Rwakatare kabla ya kuzikwa

Mchungaji Rwakatare azikwa, Kanisa lake lakerwa na uzushi

Na Mwandishi Wetu

MWANZILISHI wa Kanisa la Mlima wa Moto (Mikocheni B Assemblies of God) Mchungaji Getrude Rwakatare (70), amezikwa jana eneo  la Kanisa hilo Mikocheni B, jijini Dar es Salaam, huku uongozi wa Kanisa hilo ukiwataka Watanzania kupuuza maneno yote yaliyozagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Mazishi ya Mchungaji Rwakatare yalifanyika jana saa 5 asubuhi na kuhudhuriwa na watu wachache wakiwemo waumini wa kanisa hilo waliopewa nafasi ya kuona kaburi hilo.

Baadhi ya Waombolezaji wachache wakiwa katika mazishi ya aliyekuwa Askofu na mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Morogoro Mama Getrude Rwakatare yaliyofanyika kwenye kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni B jijini Dar Ea salaam leo.

Akizungumza wakati wa mazishi hayo mmoja kati ya wazee wanne wa Kanisa hilo na mmoja wa viongozi, Dkt. Furaha Mramba, aliwataka Watanzania kupuuza uzushi uliosambazwa mitandaoni ikiwemo kwamba kwenye kaburi hilo litazikwa jeneza tupu na mwili wa mama (Mchungaji Rwakatare) hautakuwemo.

Dkt. Furaha alisema walisikia maneno mengi sana na kwamba uongozi wa hospitali (Ulipohifadhiwa mwili wake) waliuandaa vizuri na waliweza kuingia wazee wanne mochwari kushuhudia mwili wake.

“Na tuliweza kumuona mama yetu (Mchungaji Rwakatare) ameandaliwa tayari kwa mazishi na mimi kama kiongozi wa Kanisa hili, kwanza nisingeweza kabisa kusema uongo,” alisema Dkt. Furaha na kuongeza;

“Ningekuwa muongo ningekuwa napita pale nahukumiwa kwamba tumeweka jiwe pale. Tuliyemzika pale ni Mama Getrude Rwakatare, ambaye ni Askofu wetu wa Kanisa la Mlima wa Moto na tumeshuhudia na tuna amani zote.

Tunashukuru uongozi mzima wa Serikali walifanya maandalizi mazuri, tunashukuru uongozi wa Bunge, wamefanya maandalizi mazuri, tunamshukuru Rais wetu, amelia na sisi na Mungu awasamehe wale wote waliosema uongo.”

Aliwataka wale waliokuwa wakisema maneno hayo wanyamaze, wamuache apumzike kwa amani kwani amezikwa Aprili 23, mwaka huu saa tano.

Kwa upande wake Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Mallya, alisema kwao huo ni msiba mzito, kwani alijifunza mambo mengi kutoka kwa Mchungaji Rwakatare. Alisema kuondoka kwa Mchungaji Rwakatare kisiwe chanzo cha mifarakano ndani ya Kanisa hilo.

“Naomba umoja katika familia, naomba umoja katika Kanisa. Yeye alisimama kama Kanisa na sisi tuendelee kusimama kama Kanisa tukionesha ushirikiano naamini kila kitu kitakuwa rahisi na tutasonga mbele kuanzia pale alipotuachia,” alisema Mchungaji Mallya.

Wakati wa mazishi hayo baadhi ya waumini wa kanisa hilo walipewa nafasi ya kushuhudia kaburi, lakini hawakuruhusiwa kushiriki mazishi hayo.

Pia baadhi ya watu walipata nafasi ya kuweka mashada kwenye kaburi la Mchungaji Rwakatare kwa uwakilishi. Walioruhusiwa kuweka mashada ni wana familia pamoja na watu wa karibu. Kati ya hao ni mama wa marehemu mchungaji Rwakatare, watoto wa Mama Rwakatare ambao waliweka shada la pamoja wakiongozwa na mtoto wa kwanza, wa marehemu, Dkt. Rose

Rwakatare.

Mama yake Mchungaji Rwakatare aliweka shada hilo kwa kushirikiana na mama yake mdogo wa marehemu na baadaye kufuatiwa na ndugu wa mchungaji Rwakatare, ambapo maua yalikuwa yakiwekwa kwa uwakilishi.

Wengine walioweka mashada ni maaskofu waliokuwa wakishikiliana moja kwa moja na marehemu katika kumtumikia Mungu. Wengine ni viongozi wa makanisa ya Mlima wa Moto. Mchungaji Rwakatare alifariki Jumatatu alfajiri kwa shinikizo la damu.